DAWASA, MADIWANI WAKUTANA KUWEKA MIKAKATI KUBORESHA HUDUMA UBUNGO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekutana na Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa Ubungo kwa lengo la kubaini changamoto ya upatikanaji wa majisafi pamoja na kuweka mikakati ya namna ya kuboresha huduma kwa Wananchi.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na Madiwani kutoka kwenye Kata ya Mburahati, Ubungo, Kimara, Makurumla, Sinza, Msigani, Makabe na Golani za Ubungo, kiliongozwa na Mstahiki Meya wa Ubungo Ndugu Jaffary Nyaigesha kilitoa nafasi kwa Madiwani kuelezea changamoto mbalimbali za huduma zilizopo kwenye Kata na mitaa yao pamoja na kuweka mikakati ya pamoja na DAWASA juu ya namna ya kuboresha huduma ya majisafi.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma Mkoa wa Dar es salaam na Pwani, Mstahiki Meya wa Ubungo Mheshimiwa Nyaigesha ameipongeza DAWASA kwa kazi kubwa iliyofanywa na inayoendelea kufanywa Ubungo ya kuboresha huduma ya majisafi, lakini alisisitiza kazi kubwa inahitajika ili kusogeza huduma ya maji kwa wananchi wote na kuhakikisha huduma inafika kwa kila Mwananchi.
“Kwa maeneo ambayo tayari miradi mikubwa imekwishakamilika, kazi kubwa ifanyike ya kusogeza huduma ya maji kwa Wananchi kwa ukaribu ili kuwapunguzia muda wa kufuata maji mbali, lakini pia kuwapa wananchi fursa ya kunufaika na uwekezaji wa Mhe. Rais,” aliongezea.
Mstahiki Meya ameeleza ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa chini ya Serikali ya awamu ya Sita ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jitihada kubwa zinahitajika za kufikisha huduma kwa wananchi wote na hivyo kazi kubwa inatakiwa kufanyika kuhakikisha huduma inaimarika kikamilifu kwa wananchi wa Ubungo.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema Mamlaka inaendelea na jitihada za kuimarisha huduma hususani kwenye vyanzo vya maji vya Ruvu Juu na Ruvu Chini ili huduma iweze kupatikana kwa uhakika na kwa muda wote.
“Kwa eneo la Ubungo, Mamlaka inaendelea na kazi ya kusambaza maji kwenye mitaa ya wananchi hususani maeneo yenye changamoto kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali waliopo. Uwekezaji uliofanyika umesaidia Wilaya ya Ubungo kupunguza changamoto za Maji zilizokuwepo miaka ya nyuma," aliongezea Mhandisi Bwire.
DAWASA inahudumia jumla ya Kata 14 na mitaa 90 katika Wilaya ya Ubungo