DAWASA SHIRIKIANENI NA JUMUIYA ZA WANANCHI KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI - WAZIRI AWESO
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameielekeza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kushirikiana na jumuiya za watumia maji katika uboreshaji wa huduma za maji katika jamii kwa kuweka taratibu wezeshi za usimamizi na uendeshaji wa miradi ya jumuiya hizo ili wananchi waweze kupata huduma endelevu.
Mhe. Aweso ametoa maelekezo hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa kisima cha Majisafi katika Mtaa wa Mafuriko, Kata ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam ambapo aliiagiza DAWASA na Mamlaka nyingine za Maji Nchini kuwa karibu zaidi na jumuiya za watumia maji na kuzisaidia katika kuboresha huduma za kwa jamii.
"Moja ya jukumu la Wizara ya Maji ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji, hivyo DAWASA na Mamlaka zote za Maji Nchini zihakikishe zinaweka taratibu nzuri za usimamizi wa miongozo ya uendeshaji huduma katika miradi hii ya kijamii hususan kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na yale yenye changamoto ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma majisafi na salama" ameeleza.
Aidha, Mhe. Aweso ameelekeza uongozi wa DAWASA kukaa na uongozi wa Kata ya Ilala ili kuona namna ya kutatua changamoto zinazohusiana na huduma ya maji ikiwemo uendelezaji wa visima vya maji vilivyopo katika Kata hiyo ya Ilala.
Naye Katibu wa Mradi wa Majisafi Mtaa wa Mafuriko Bungoni Bwana Gidion Innocent Nkwita ameishukuru Wizara ya Maji na DAWASA kwa ushirikiano mzuri katika usimamizi wa ujenzi mradi na ushauri wa kitaalamu wa mara kwa mara katika kutatua changamoto mbalimbali za maji.
"Tunapata ushirikiano mzuri toka DAWASA hususan kwenye changamoto za matengenezo ya miundombinu na tunawasihi waendelee kuwa karibu zaidi na jumuiya hii ili Wananchi waendelee kupata huduma maji kwa uhakika." Ameeleza.
Mradi huu ni miongoni mwa miradi ya Maji iliyokabidhiwa DAWASA kutoka Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Mwaka 2020 na una jumla ya wateja 222 ambao wanahudumiwa na Jumuiya ya watumiaji maji Mtaa wa Mafuriko, Kata ya Ilala kwa usimamizi wa DAWASA.