Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
MBUNGE WA SEGEREA APONGEZA KASI MRADI WA MAJI BANGULO
30 Dec, 2024
MBUNGE WA SEGEREA APONGEZA KASI MRADI WA MAJI BANGULO

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonna Kamoli ameishukuru Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji wa Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo).

Bonna amesema kwa kasi na kwa ufanisi mzuri inachagiza matumaini ya upatikanaji wa maji kwa siku za karibuni. 

Amesema wananchi wa Jimbo la Segerea na maeneo ya jirani matumaini yao makubwa ni kuona mradi huu unakamilika na wananchi wanaanza kupata maji, kwa kuwa tatizo la maji kwao ni kubwa la muda mrefu. 

"Mradi huu ni mkubwa na utahudumia wakazi wengi sana, kukamilika kwake kutaleta ahueni kubwa kwa wananchi wengi ambao hawana maji. Niwapongeze sana DAWASA kwa muda mfupi mradi umetekelezwa kwa sehemu kubwa na kazi iliyobaki ni ndogo ya kukamilisha," amesema Bonna.

Amewataka viongozi wa Kata na mitaa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ili wapate urahisi wakati wa utambuzi wa maeneo ya kupitisha maji kwa wananchi kwani itarahisisha usambazaji wa huduma kwa haraka na kwa watu wote. 

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kazi kubwa imefanyika katika utekelezaji wa mradi huu na mpaka sasa utekelezaji umefikia asilimia 95, zimebaki asilimia 5 tu za kukamilisha. 

"Kuhusu kazi ya ulazaji wa mabomba, mpaka sasa kati ya kilomita 119 za ulazaji wa mabomba tumefanikiwa kulaza mabomba kwa kilomita 118.2 bado mita 800 tu kukamilisha zoezi hili," amesema Mhandisi Bwire.  

Amesema kazi ya ujenzi wa kituo cha kusukuma maji imekamilika na zoezi lililobaki ni ufungaji wa pampu za kusukuma maji. 

"Tunaishukuru sana Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa namna hii wa Bilioni 36 kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa maeneo haya ya Dar es Salaam ya Kusini nao wanapata maji kwa uhakika bila usumbufu wowote," amesema Mhandisi Bwire

Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Bangulo,  Goodluck Mwele ameipongeza Mamlaka kwa jitihada kubwa za kutekeleza mradi huu kwa kasi na kwa ufanisi na hii inasaidia kuwapa imani wananchi kuwa Serikali haiko kimya katika suala la maji na kazi imefanyika na inaonekana. 

Amesema ushirikiano umekuwa ni mzuri kwa muda wote na tumefanikiwa kulinda miundombinu yote ya ujenzi na tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi kushiriki katika ulinzi wa miundombinu ya maji. 

"Shauku ya wananchi ni kuona mradi unakamilika na wanapata maji na kwa jitihada hizi ni wazi kuwa hivi karibuni wananchi wataanza kunufaika na huduma ya majisafi," amesema Mwele.

Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya Sinohydro Construction - Stecol JV kwa gharama ya Shilingi  Bilioni 36 na unatarajia kunufaisha zaidi ya wakazi 450,000 katika Wilaya za Ilala, Ubungo, Temeke na Kisarawe katika Kata za Kitunda, Kipunguni, Mzinga, Pugu Station, Kiluvya, Msigani pamoja na kuongeza msukumo wa maji katika maeneo ya Kata ya Kinyerezi.