SINZA C NA D WAIMARISHIWA HUDUMA YA MAJISAFI

Wananchi waishukuru DAWASA kukamilisha mradi.
Wananchi mbalimbali wa mitaa ya Sinza C na D wameishukuru DAWASA kwa kukamilisha mradi uliolenga kuimarisha huduma ya majisafi katika mtaa wao hali inayowafanya kupata huduma ya majisafi waliyoikosa kwa kipindi kirefu.
Ndugu Halima Maulid mkazi wa Sinza D ameeleza ni kipindi kirefu kimepita bila kuwa na huduma ya maji, lakini walipata matumaini baada ya DAWASA kuwasikiliza kilio chao na kutekeleza mradi na kwasasa wanapata huduma ya maji.
"Ilifika kipindi tukakata tamaa ya kuwa na huduma ya majisafi, tunaishukuru DAWASA kwakua wasikivu na kutuletea mradi ambao umemaliza changamoto ya ukosefu wa maji katika mtaa wetu, kwanzia jna tumeona wengi tunapata maji baada ya kipindi kirefu kupita" ameeleza ndugu Halima.
Meneja wa Mkoa wa kihuduma DAWASA - Magomeni ndugu, Julieth John ameeleza kuwa kwasasa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wameanza kupata huduma ya maji.
"Mradi huu ulihusisha uchimbaji na ulazaji wa bomba zenye ukubwa wa inchi 6 kwa umbali wa kilomita 1 na tumefanya majaribio ya mradi na kupata matokeo chanya ambapo wananchi wameanza kupata huduma ya majisafi walioikosa kwa muda mrefu" ameeleza ndugu, Julieth.
Mradi huu unaogharimu kiasi cha Tsh. Milioni 69 utanufaisha wakazi takribani 2000 katika mitaa ya Sinza C na D walioanza kupata huduma ya majisafi.