Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
AGIZO LA MAKAMU WA RAIS SOKO LA ILALA WAANZA KUTEKELEZWA
06 Jun, 2024
AGIZO LA MAKAMU WA RAIS SOKO LA ILALA WAANZA KUTEKELEZWA

DAWASA yaja na mpango uboreshaji Usafi wa Mazingira soko la Ilala.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais Mh. Philip Mpango alilolitoa hivi karibuni ya kutatua changamoto ya utiririshaji majitaka katika Soko la Ilala.

Makamu wa Rais alitoa agizo hilo wakati wa zoezi la usafi wa Jiji la Dar es Salaam katika soko la Ilala ambapo aliitaka DAWASA kushughulikia tatizo la utiririshaji wa majitaka ndani ya muda mfupi.

Akizungumzia utekelezaji wa agizo hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Usafi wa Mazingira DAWASA, Mhandisi Lydia Ndibalema amesema kuwa tathimini ya awali imeshafanyika baada ya kufanya ukaguzi wa miundombinu ya majitaka katika soko hilo na kubaini tatizo kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi.

"Tumeshafanya tathmini ya awali ya ukaguzi wa  miundombinu yetu, tumebaini kuwepo kwa changamoto ya uzibaji wa chemba iliyosababishwa na kazi ya ujenzi wa barabara inayoendelea katika mitaa ya Ilala, ambapo mkandarasi aliondoa mifuniko ya chemba za majitaka na kusababisha taka ngumu kujaa katika chemba," ameeleza Mhandisi Ndibalema.

Ndibalema ameongeza kuwa wameanza kufanya kazi kwa ushirikiano na Tanroad pamoja na mkandarasi wa barabara kwa kusafisha chemba hizo na kuziwekea mifuniko ya chuma ili kutoruhusu taka ngumu kuingia katika chemba na kazi hiyo inayotarajia kufanyika ndani ya wiki hii.

Mhandisi Mary Njau kutoka kampuni ya Ujenzi ya Osaka inayotekeleza ujenzi wa barabara ameeleza kuwa wamekwisha pokea mifuniko ya chuma na ndani na kazi ya kuirudishia kwenye chemba za majitaka imeanza kwa kasi.

Mwenyekiti wa mtaa wa Bungoni Ndugu Ally Mshauri akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa ilala, ameipongeza DAWASA kwa mwitikio wa haraka na kuwa wasikivu na kufika kukagua miundombinu yao.

"Utayari huu wa DAWASA unatoa matumaini kwa wafanyabiashara sokoni hapa kwani wakati mifuniko ya chuma itapowekwa, taka ngumu hazitaingia na kuziba chemba hali iliyofanya majitaka kutirirka sokoni na kusababisha hatari ya magonjwa ya mlipuko," ameeleza Ndugu Mshauri.