Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MSAKUZI - MACHIMBO HADI MAKABE KUKAMILISHIWA MRADI WA MAJI IFIKAPO JULAI 2026
05 Mar, 2026
MSAKUZI - MACHIMBO HADI MAKABE KUKAMILISHIWA MRADI WA MAJI IFIKAPO JULAI 2026

Wananchi wa Mtaa wa Machimbo, Kata ya Mbezi, wameonesha furaha yao kufuatia utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya majisafi wa Msakuzi–Machimbo hadi Makabe, unaolenga kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji iliyodumu kwa muda mrefu katika eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Machimbo, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Ndugu Said Suleiman Diuchile, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuamua kutekeleza mradi huo ambao una matarajio makubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

“Mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Machimbo napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Jumaa Aweso pamoja na DAWASA kwa kutekeleza mradi huu ambao tunaamini utakwenda kumaliza kilio chetu cha muda mrefu cha maji,” amesema Diuchile.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi wa DAWASA Ubungo, Mhandisi Sheka Omar, amesema utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri kulingana na ratiba iliyopangwa. Amesema kwa sasa kazi ya ulazaji wa mabomba katika eneo la Machimbo inaendelea kwa umbali wa kilomita 5.2.

“Kwa sasa tupo katika hatua ya ulazaji wa mabomba ya inchi 6 na inchi 3, na kazi inaendelea kwa kasi kubwa ili kuhakikisha tunafikia lengo la kuukamilisha mradi huu kwa wakati kama ilivyoainishwa na Mamlaka,” amesema Mhandisi Sheka.

Amefafanua kuwa changamoto ya maji katika eneo hilo imesababishwa kwa kiasi kikubwa na miinuko ya kijiografia, hali iliyokuwa ikifanya baadhi ya mitaa kukosa huduma ya uhakika. Hata hivyo, ameongeza kuwa mradi huo ukiwa katika asilimia 67 ya utekelezaji, unatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 2026 na kuanza rasmi kutoa huduma kwa wananchi.

“Mitaa mingi ya Machimbo imekuwa haipati maji ya uhakika kutokana na miinuko, lakini mradi huu utakapokamilika tatizo hilo litakuwa historia,” ameongeza.

Naye Bi. Hyasintha Mabula, mkazi wa Mtaa wa Kigai, Machimbo, ameipongeza DAWASA kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo. Amesema wakazi wamekuwa wakishuhudia kila siku watumishi wa mamlaka hiyo wakiendelea na kazi ya uchimbaji na ulazaji wa mabomba katika maeneo yao, jambo linalowaongezea imani kuwa mradi utakamilika kwa wakati.

Kukamilika kwa mradi wa Msakuzi–Machimbo hadi Makabe kunatarajiwa kunufaisha takribani wakazi 500 kutoka mitaa ya Machimbo Tanzanite, IQ, Igoma, Darajani, Bethsaida, Msikitini, Sabato Road, Pande Road pamoja na Kigai, hatua itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.