Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
AGIZO LA WAZIRI AWESO UBORESHAJI HUDUMA YA MAJI MANGA LAANZA
20 Nov, 2024
AGIZO LA WAZIRI AWESO UBORESHAJI HUDUMA YA MAJI MANGA LAANZA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza zoezi la kuwaandikisha wakazi wa Kijiji cha Manga, Kata ya Mkata, Wilaya ya Handeni Vijijini ili kuwapatia huduma ya majisafi kwa mkopo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso alilotoa kwa DAWASA hivi karibuni.

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) CPA (T) Ritamary Lwabulinda amesema kuwa Kijiji cha Manga ni miongoni mwa vijiji vinavyotumia huduma ya naji kwa kupitia  Mtambo wa Maji Wami na usambazaji wa Maji hufanyika kupitia vizimba vya maji (vioski).

“Kutokana na wakazi wengi wa Kijiji cha Manga kutomudu ulipaji wa gharama za maunganisho ya huduma ya Majisafi, Mhe. Waziri wa Maji alielekeza DAWASA kuwaunganishia huduma ya maji kwa mkopo wakazi wa Manga. Hivyo Mamlaka tumeanza utekelezaji wa zoezi hilo kupitia Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Manga na hadi sasa  kaya takribani 41 zimwshaandikishwa kutoka vitongoji vya Majengo, Kwa Maloko, Gombelo, Nkundusi, Mwananyamala, Mapinduzi na Majani Mapana kwa ajili ya kupata huduma hiyo” alisema Lwabulinda

Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mkata, Bw. Omari Salim ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuwaletea mpango huu wa kuwaunganishia maji kwa mkopo. 

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri wa Maji kwa kuwajali Wananchi wenye kipato cha chini, ameonesha kutujali ili tuweze kupata huduma hii muhimu”. Amesema Bw. Omari.

Kwa upande wake, Mkazi wa Kijiji cha Manga Bi. Hadija Mdoe ameipongeza DAWASA kwa kuchukua hatua za haraka katika utekelezaji wa agizo la Mhe. Waziri Aweso.

“Kwa kweli tunaipongeza DAWASA, tumeona ni siku kadhaa tu zimepita tangu Waziri Aweso alipopita hapa na kutoa maagizo na leo wamekuja kufanya kikao na wakazi wa Manga na kuanza kuandikisha majina ili kuanza utaratibu wa huduma hiyo ya maunganisho.”

Kijiji cha Manga kina jumla ya wakazi 10,552 katika kaya 6,500 ambao kwa sasa wanapata huduma ya maji kupitia vizimba 17 vinavyosambaza huduma ya maji katka Kijiji hicho.