BANGULO WAIMARISHIWA MIUNDOMBINU KUPUNGUZA UPOTEVU WA MAJI

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na zoezi la uboreshaji wa miundombinu ya mabomba ya maji ili kuimarisha huduma na kudhibiti upotevu wa maji katika maeneo mbalimbali ya Mtaa wa Bangulo, Kata ya Pugu Stesheni, Wilaya ya Ilala.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhandisi Adam Makindai, kutoka Mkoa wa Kihuduma DAWASA Ukonga amesema uboreshaji huo umekusudia kuimarisha huduma kutokana na kuongezeka hali ya uvujaji na upotevu wa maji katika eneo hilo.
"Maboresho haya yanahusisha ubadilishaji wa mabomba chakavu yaliyorithiwa kutoka katika Mradi wa Jumuiya za Watumia Maji kwa kuondoa mabomba ya kipenyo cha inchi 1.5 na kuweka mapya ya inchi 2 kwa umbali wa mita 1,500 katika maeneo ya Ubalozini, Kwa Msafiri, Mji Mpya, Kwa Mwandika na Kwa Adamu ambapo zaidi ya wateja 500 watanuifaika na maboresho hayo." amefafanua Mhandisi Makindai.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bangulo, Goodluck Mwele ameishukuru DAWASA kwa hatua ya uboreshaji wa miundombinu kutokana na hali ya uvujaji kuwa kubwa katika maeneo mengi ya Mtaa huo.
"Kwa niaba ya wananchi wa Mtaa wa Bangulo tunawashukuru DAWASA kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Maji ya kutuletea huduma ya maji na uboreshaji wa miundombinu ya Mradi uliokuwa wa Jumuiya ya Watumia Maji kwa kubadili mabomba yaliyochakaa na kuweka mapya ambayo yatasaidia kuondoa changamoto kubwa ya Uvujaji wa maji katika Mtaa wetu" Amesema Mwele.
Mkazi wa Mtaa wa Amani Bangulo, Amina Mkundela ameipongeza DAWASA kwa kuboresha miundombinu hiyo kwani ilikuwa inaharibu barabara za mitaa hiyo.
"Tumefurahi maji ni mengi sana lakini maji mengi yanamwagika mtaani sababu mabomba ni ya zamani sana yamechakaa hivyo yanapasuka kila siku na kutuharibia mazingira lakini sasa tunaona juhudi za DAWASA kutuondolea changamoto hiyo." Amesema Amina.
Mtaa wa Bangulo ni miongoni mwa maeneo yanahudumiwa na maji kutoka katika Mradi mpya wa Dar es Salaam ya Kusini unaotekelezwa na DAWASA ambao tayari umekamilika na unaendelea na hatua za majaribio ya usambazaji maji pamoja na zoezi la maunganisho ya wateja wapya katika maeneo hayo.