Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
BILIONI 1.8 KUSUKUMA HUDUMA ZA MAJITAKA KIBAHA
28 Jul, 2026
BILIONI 1.8 KUSUKUMA HUDUMA ZA MAJITAKA KIBAHA

Ujenzi wa mtambo wa kisasa wa kuchakata majitaka unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika eneo la Mitamba, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, umefikia asilimia 52 ya utekelezaji.

Mradi huo unatarajiwa kuwa suluhisho muhimu katika kuboresha usafi wa mazingira, afya ya jamii na mfumo wa usimamizi wa majitaka kwa wakazi wa Kibaha na maeneo ya jirani.

Mradi huo wa kimkakati unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.8 kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia, huku ukitarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu.

Baada ya kukamilika, mtambo huo utakuwa na uwezo wa kuchakata zaidi ya lita 220,000 za majitaka kwa siku, hatua inayolenga kupunguza uchafuzi wa mazingira, kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha huduma za usafi wa mazingira katika maeneo yanayokua kwa kasi.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Aden Mwaseba, amesema ujenzi unaendelea vizuri huku mkazo ukiwekwa katika kuhakikisha kazi zote zinazingatia viwango vya ubora vilivyowekwa.

Amesema kwa sasa mkandarasi anaendelea na ufungaji wa mabati ya kufungia zege (formwork) pamoja na ujenzi wa kuta za tenki la kupokelea majitaka (STT).

Kwa mujibu wa Mhandisi Mwaseba, ujenzi wa kuta za kichanja cha kukaushia tope (Sludge Drying Bed – SDB) umekamilika, jambo linaloonesha hatua nzuri iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.

“Mradi umefikia asilimia 52 ya utekelezaji na unaendelea vizuri. Tunahakikisha kila hatua inazingatia viwango vya ubora vilivyowekwa ili kuukamilisha kwa wakati na kuanza kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Mhandisi Mwaseba.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha uwezo wa kuchakata majitaka, kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira na kuboresha afya za wananchi, sambamba na kuongeza ufanisi katika huduma za usimamizi wa majitaka.

Aidha, amesema mradi huo utasaidia ukuaji wa miji kwa kuzingatia viwango vya usafi na uhifadhi wa mazingira, hususan katika maeneo yanayokabiliwa na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Lumumba, Amos Masamba, ameipongeza DAWASA kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo, akisema wananchi wana matumaini makubwa ya kuuona ukikamilika kwa wakati.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Kibaha, hasa katika kuboresha usafi wa mazingira na kuongeza ufanisi wa huduma za majitaka.

“Mradi huu ni wa muhimu sana kwa maendeleo ya Kibaha. Ukikamilika utaboresha usafi wa mazingira, kuongeza ufanisi wa huduma za usimamizi wa majitaka, kupunguza gharama za uendeshaji kwa watoa huduma na kuchangia kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira yetu,” amesema Masamba.

Mradi huo unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya majitaka na kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira katika Kibaha na maeneo yanayozunguka.