BILIONI 2.2 KUMALIZA TATIZO LA MAJI MSUMI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imetenga Shilingi Bilioni 2.2 kutafuta Suluhu ya tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji katika mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi, wilayani Ubungo.
Mradi mkubwa na wa kimkakati katika mtaa wa Msumi ulioanza kutekelezwa Aprili mwaka huu, unatarajia kukamilika Januari mwakani huku zaidi ya wakazi 47,000 wa Mitaa ya Msumi A, Msumi B, Msumi C pamoja na Tegeta A watanufaika.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, msimamizi wa mradi, Mhandisi Aziz Namanga amesema mradi unaendelea kwa kasi na kuwahakikishia wananchi wa eneo la Msumi huduma ya majisafi na salama pindi mradi utakapokamilika.
"Mradi huu umehusisha uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya maji yenye ukubwa wa inchi 6, 4, 2, na 1 kwa jumla ya kilomita 14.9, ambapo hadi sasa, kilomita 11 za mabomba tayari zimekwishalazwa na kazi ya ulazaji bomba imefikia asilimia 76," amesema Mhandisi Namanga.
Namanga amesema mbali na ulazaji wa mabomba, mradi huu pia unahusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 500,000, pamoja na mnara wa tenki hilo wenye urefu wa mita 12, ujenzi wa vituo 12 vya kuchotea maji, ufungaji wa pampu na uwekaji wa transfoma ya umeme ambayo ni muhimu kwa uendeshaji wa mifumo ya kusambaza maji.
Ndugu Mohammed Issa, mkazi wa Msumi ameipongeza DAWASA kwakuja na mradi huu kwani awali walipata changamoto ya huduma ya maji na kusababisha gharama za maisha kuongezeka na kuhatarisha afya zao kwa kutumia maji yasiyo na uhakika wa usalama wake.
"Hapa kwetu tumekuwa na changamoto ya huduma ya maji, gharama za maisha zilipanda sana kwa kununua maji kwa bei ghali, kwa mwezi unaweza tumia hadi Shilingi 200,000 kununua maji tu, lakini pia ni maji ambayo hatuna uhakika na usalama wake jambo ambalo limehatarisha afya zetu," amesema Ndugu Issa.