Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAZIRI AWESO ATEKELEZA AHADI, DC MSANDO AMPONGEZA
05 Dec, 2025
WAZIRI AWESO ATEKELEZA AHADI, DC MSANDO AMPONGEZA

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amekabidhi Shilingi 5 milioni na mifuko 100 ya saruji kwa shule ya msingi Msumi Wilayani Ubungo ili kukamilisha ujenzi wa madarasa matatu.

Mchango huo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa tarehe 28.11.2025 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara mtaa wa Msumi.

Mchango huo umekabidhiwa leo tarehe 3.12.2025 na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa niaba ya Waziri Aweso kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo (DC), Mhe. Albert Msando.

Msando amemshukuru Waziri Aweso kwa kuwa mwepesi kuwasililiza na kutoa ahadi hiyo ambayo ameitekeleza kwa wakati.

"Nimshukuru Mhe. Aweso, Waziri wa maji kwa kutekeleza ahadi yake hii ambayo leo tunakabidhiwa na DAWASA hapa shuleni, mimi mwenyewe binafsi nitasimamia fedha hizi kikamilifu ili madarasa haya yaweze kukamilika kwa wakati na kutumika ifikapo muhula mpya wa masomo mwezi Januari," amesema Msando.

Msando amesema kukamilika kwa madarasa haya na kuanza kutumika kutasaidia kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi kusomea katika darasa moja ambapo kwasasa kuna darasa lenye wanafunzi hadi 165 badala ya kiwango kinachohitajika cha wananfunzi 45 hadi 50.

Naye Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkurugenzi wa Miradi, Mhandisi Ramadhan Mtindasi amesema sekta ya maji itaendelea kutoa ushirikiano kwa sekta nyingine kama vile elimu ili kuchochea maendeleo ya wananchi inayowahudumia.

"Hapa Msumi pia tunatekeleza mradi wa maji, tunapata ushirikiano mkubwa sana toka serikali ya mtaa na wananchi, tunashukuru sana kwa hilo, tunaimami tukiwaboreshea watoto hawa Mazingira mazuri ya kusoma tunaandaa taifa bora badae," amesema Mhandisi Mtindasi.

Kwa upande wake, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Msumi, Ndugu Paulo Mdachi amemshukuru Waziri wa Maji kwakutekeleza ahadi yake na kuchangia ukamilishaji wa madarasa katika shule hiyo kwani kutachochea utoaji wa elimu bora na mazingira rafiki ya kujifunzia.

Shule ya msingi Msumi inayopatikana Wilaya ya Ubungo ina jumla ya wananfunzi 2,465, wanafunzi wa kiume wakiwa 1,199 na wakike wakiwa 1,266.