BOKO MAWENI KUIMARISHIWA HUDUMA ZA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefanikiwa kuwafikia wananchi 230 wa Mtaa wa Boko Maweni, Kata ya Bunju, Wilaya ya Kinondoni na kutoa uhakika wa upatikanaji wa Majisafi kupitia mradi wa maji wa Dovya Mapokezi.
Mradi huu unahusisha ulazaji wa mabomba ya inchi 4 na inchi 2 kwa umbali wa kilomita 7.5, kwa hatua inayolenga kupunguza changamoto ya msukumo mdogo wa maji na kutatua changamoto ya ukosefu wa maji katika eneo hilo.
Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA Mivumoni, Bi Victoria Masele amesema dhamira ya Mamlaka ni kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi kwa haraka.
"Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya majisafi na salama, na jukumu hilo lipo mikononi mwetu na tulitekeleze," amesema Bi Victoria.
Ameongeza kuwa, mojawapo ya changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huu ni ugumu wa ardhi inayochimbwa kwa ajili ya kulaza mabomba.
"Mamlaka imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa wakati. Licha ya zoezi la uchimbaji wa mabomba kuwa gumu kutokana na uwepo wa miamba ya kokoto, tumejipanga kutumia vifaa vyenye uwezo mkubwa ili kuharakisha kazi," ameeleza Bi Victoria.
DAWASA inaendelea na juhudi zake za kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa wananchi wake.
Aidha, Mamlaka inawashirikisha wananchi kwa njia mbalimbali, ikiwemo kampeni ya nyumba kwa nyumba, mikutano ya hadhara na mitandao ya kijamii ili kuhakikisha wanatambua juhudi zinazoendelea katika kuboresha huduma za maji Jijini Dar es Salaam.