BOMBANI, PUGU MPAKANI HADI BANGULO WAITWA KUUNGANISHIWA MAJI

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewataka wakazi katika Kata za Pugu, Gongolamboto na Pugu Stesheni Wilayani Ilala kujitokeza na kuunganishiwa huduma ya maji baada ya kukamilika kwa mradi wa Usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) na miradi mingine midogo ya kusogeza mtandao wa huduma majumbani kwa wateja.
Melkiad Lyamuya, Afisa huduma kwa wateja DAWASA - Ukonga ameeleza hayo wakati wa kampeni ya nyumba kwa nyumba kuwafikia wateja kupitia dawati la huduma kwa wateja linalofunguliwa eneo la Mwanapindi, Kata ya Pugu Stesheni.
"Kwasasa kazi ya kusogeza mtandao wa miundombinu ya huduma imekamilika na huduma inapatikana hususan Mtaa wa Bombani kwa Kata ya Pugu, Mitaa ya Pugu Mpakani, Pugu Kichangani na Bangulo kwa Kata ya Pugu Stesheni. Vilevile katika mitaa ya Gongolamboto, Ulongoni pamoja na Mtaa wa Markaz katika Kata ya Ukonga, hivyo tunawahimiza wakazi wa maeneo hayo kujitokeza na kuleta maombi yao ili waunganishiwe huduma.," amesema Ndugu Lyamuya.
Aidha, Ndugu Lyamuya ametumia wasaa huo kuwahimiza Wananchi kulinda miundombinu ya maji katika maeneo yao na kutoa taarifa DAWASA kituo cha huduma kwa wateja kupitia namba 181 wanapoona shughuli zinazoathiri miundombinu ya maji au uvujaji.
Jumla ya wakazi 119 wamejitokeza na kuhudumiwa ambapo 81 wamefika kwenye Dawati la huduma na wengine 38 wametembelewa majumbani kupatiwa elimu na kuongeza uelewa juu ya huduma za DAWASA.