Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
CHALINZE: DAWASA YATAMBUA MCHANGO WA WANAFUNZI KUTUNZA MAZINGIRA
12 Oct, 2026
CHALINZE: DAWASA YATAMBUA MCHANGO WA WANAFUNZI KUTUNZA MAZINGIRA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewapongeza wanafunzi waliohitimu Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, kwa mchango wao katika shughuli za utunzaji wa mazingira kupitia klabu ya shule hiyo.
‎
‎Wanafunzi hao wametambuliwa wakati wa mahafali ya 18 ya Kidato cha Nne ya mwaka 2026, ambapo DAWASA iliwapatia vyeti na madaftari kama motisha ya kuendelea kushiriki katika uhifadhi wa mazingira na rasilimali za maji.
‎
‎Afisa Mawasiliano wa DAWASA, Prisca Makenya, amesema kutambua mchango wa wanafunzi hao ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha vijana wengine kushiriki katika shughuli za klabu na kuzingatia matumizi sahihi ya maji.
‎
‎Amesema DAWASA pia imeahidi kutoa tanki la kuhifadhia maji kwa shule hiyo ili kusaidia uhifadhi na matumizi bora ya maji.
‎
‎Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Diwani wa Kata ya Bwilingu, Lawrence Peter Singau, amewapongeza wahitimu kwa hatua waliyofikia na kuwataka kuongeza bidii na nidhamu katika maandalizi ya mtihani wao wa mwisho.
‎
‎Mwalimu anayesimamia Klabu ya Mazingira shuleni hapo, Philemon Hechei, ameishukuru DAWASA kwa kuendelea kutoa elimu ya majisafi na usafi wa mazingira pamoja na vifaa vinavyosaidia shughuli za shule.
‎
‎Kwa upande wao, wahitimu wameiomba DAWASA kuendelea kutoa elimu ya mazingira ili kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi kuelewa umuhimu wa kulinda maji na mazingira.
‎
‎DAWASA imesema inaendelea kushirikiana na shule 12 kupitia programu za Klabu za Mazingira, zinazolenga kuwajenga vijana kuwa mabalozi wa maji, usafi na utunzaji wa mazingira katika jamii.