DAWASA, EXIM BENKI YA KOREA WAKUTANA, WAKUBALIANA KUIMARISHA HUDUMA ZA MAJI DAR
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Majisafi na Usafiri wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Romanus Mwang'ingo amekutana na ujumbe kutoka Benki ya Exim ya Korea ili kuzungumza ni kwajinsi gani kwa pamoja wanaweza kushirikiana kutoa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi.
"Lengo la kukutana kwetu ni kuboresha urafiki uliodumu kwa muda mrefu kati ya DAWASA na Benki ya Exim kutoka Korea, lakini zaidi kuwapitisha katika mipango yetu ili kwa pamoja tuone wapi tunaweza kushirikiana na wananchi wakapata huduma hususani utekelezaji wa miradi mikubwa na yakimkakati," amesema Mhandisi Mwang'ingo.
Mhandisi Mwang'ingo amesema ipo miradi mikubwa na ya kimkakati ambayo ikitekelezwa na kukamilika itasaidia sana wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, miradi kama vile kutoa maji Mto Rufiji, Mradi wa Kuongeza uwezo wa kuzalisha maji katika mtambo wa Ruvu chini na mradi wa Usafi wa Mazingira Buguruni, hivyo ni vyema wakakutana na wadau kama hawa kuwashirikishaa mipango na kuona ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu kutoka Benki ya Exim ya Korea, Ndugu Kim Kyeang - gu amesema Benki ya Exim Korea imeendelea kuwa na utayari kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha huduma za jamii na wataangalia ni wapi wataweza kushirikiana na DAWASA kuboresha huduma.
"Tumepitishwa katika mipango ya DAWASA, tutakaa na kuchambua vyema kuona ni wapi tunaweza tukashirikiana kuboresha huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa wananchi tukitambua huduma ya majisafi ni kipaumbele kwa wananchi," amesema Ndugu Kim.
