Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA HAINA DENI LA HUDUMA YA MAJI KWA WAKAZI MTAA WA MBAGALA
12 Oct, 2024
DAWASA HAINA DENI LA HUDUMA YA MAJI KWA WAKAZI MTAA WA MBAGALA

Katika kuendelea kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja 2024, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea kuadhimisha vyema wiki ya huduma kwa wateja kwa kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi katika Mtaa wa Mbagala.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa Miradi DAWASA Mbagala, Alex Mwanja amebainisha ya kuwa mtaa wa Mbagala ni miongoni mwa maeneo yanayohudumiwa na DAWASA ambayo hayakuwa na huduma ya maji kwa kipindi kirefu hivyo kuilazimu Mamlaka kuwekeza nguvu kubwa kuboresha huduma ya maji katika mtaa huo kwa kulaza bomba zenye ukubwa wa inchi 3 kwa umbali wa mita 300 na inchi 2 kwa umbali wa kilomita 3.7 ili kuimarisha Hali ya upatikanaji wa huduma.

"Mtaa wa Mbagala ulikuwa hauna huduma ya maji kwa takribani miaka 4 hivyo sisi kama DAWASA tunayofuraha tunapoadhimisha wiki hii ya huduma kwa wateja wakazi wa mtaa wa Mbagala wanapata huduma ya maji" ameeleza Mhandisi Mwanja

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mbagala ndugu Ghalib Mkiena ameishikuru DAWASA kwa kuboresha huduma ambayo ilikosekana kwa kipindi kirefu katika mtaa huo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa mamlaka nyakati zote watakapohitajika.

"Kwa niaba ya wananchi wa mtaa wa Mbagala tunatoa shukrani zetu kwa DAWASA kwa kuendelea kuwajali na kuwathamini wateja wake. Kwa sasa tunafuraha baada ya huduma kurejeshwa tuliyoikosa kwa miaka 4. Tumepitia changamoto nyingi sana za maji ila kwa sasa tunavyoona yanatoka tunaipongeza na kuishukuru DAWASA hakika na sisi tunaadhimisha vyema wiki ya huduma kwa wateja na maji kwa masaa yote" amesema Mkiena

Mtaa wa Mbagala una wakazi takribani 300 na hupata huduma ya majisafi kupitia Mtambo wa uzalishaji maji Mtoni.