DAWASA, IRUWASA WABADILISHANA UZOEFU USIMAMIZI VIKUNDI KAZI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Iringa (IRUWASA) kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya usimamizi wa vikundi kazi (Special Groups).
Miongoni mwa maeneo waliyobadilishana uzoefu na kupewa kipaumbele ni eneo la usomaji wa mita za maji, Usafi wa mazingira, uunganishaji wa maunganisho mapya pamoja na udhibiti wa mivujo ya maji.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Meneja Fedha DAWASA, Leon Lutego, amesema mafunzo hayo yamekuwa fursa muhimu kwa mamlaka kupata mbinu mpya za kuendesha na kusimamia vikundi kazi vitakavyosaidia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
“Ziara kama hizi zinatupa maarifa zaidi kuhusu namna ya kuendesha na kusimamia vikundi maalumu ambavyo tunategemea vilete mafanikio chanya katika huduma tunayotoa,” amesema Lutego.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa IRUWASA Ndugu Edwin Hyela, ameipongeza DAWASA kwa hatua ya kujifunza kutoka Mamlaka nyingine akisema inalenga kuboresha huduma na usimamizi wa Vikundi kazi vitakavyoimarisha huduma na kusogeza kuboresha ufanisi mahala pa kazi.
DAWASA iimeanza utekelezaji wa baadhi ya majukumu yake kupitia vikundi kazi kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi, kupunguza muda wa kushughulikia changamoto na kuboresha huduma za kwa Wananchi.
