DAWASA, KASHWASA WABADILISHANA UZOEFU UZALISHAJI, USAMBAZAJI MAJI

Timu ya uzalishaji na usambazaji maji ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imetembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA), kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika sekta ya uzalishaji na usambazaji maji.
Ziara hiyo ya mafunzo imehusisha mafunzo ya kiufundi na ukaguzi katika mtambo wa uzalishaji maji wa Ihelele unaohudumia wakazi wa mikoa sita Mwanza, Shinyanga, Singida, Geita, Tabora na Simiyu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kiongozi wa timu ya DAWASA, Mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji maji, Mhandisi Leonard Msenyele amebainisha ziara hiyo imekuwa chachu ya kujifunza mbinu mpya za kiufundi zitakazosaidia kuboresha huduma katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani.
“Kila ziara kama hii hutupa nafasi ya kuimarisha maarifa na kuongeza ubunifu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya majisafi na salama kwa wakati,” amesema Mhandisi Msenyele.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA, Mhandisi Patrick Nzamba akizungumza wakati wa mapokezi ameipongeza DAWASA kwa jitihada za kutaka kujifunza na kuchukua uzoefu kutoka kwa wengine lakini pia kuhimiza ushirikiano wa taasisi.
“Tunaamini kushirikiana na kubadilishana uzoefu na taasisi nyingine za maji nchini ni hatua muhimu ya kuongeza ufanisi na kuimarisha huduma kwa wananchi,” amesema Mhandisi Nzamba.
Ziara za mafunzo ni sehemu ya mikakati ya DAWASA katika kuboresha huduma za maji kupitia ushirikiano wa kitaasisi na kujenga uwezo endelevu wa kiutendaji.