MILIONI 237 KUWABORESHEA HUDUMA YA MAJI KINZUDI

Wakazi zaidi ya 500 wa mtaa wa Kinzudi, Kata ya Goba, Wilaya ya Ubungo wataanza kunufaika na maboresho ya huduma ya majisafi yanayonywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es es Salaam (DAWASA).
Maboresho haya yanafanyika baada ya uhitaji mkubwa wa huduma ya maji katika eneo hilo ambalo lilikuwa likipata huduma ya maji kwa msukumo mdogo.
Akizungumzia maboresho yaliyofanyika, Mhandisi Jelson Charles amesema kazi hii upo mbioni kukamilika na ifikapo mwishoni mwa Agosti 2025 wananchi wa mtaa wa Kinzudi watasahau changamoto ya uhaba wa maji.
"Baada ya kupokea taarifa, upungufu wa huduma katika mtaa huu, Mamlaka ilijiridhisha na kuja na mradi wa kuboresha msukumo wa maji ambao umehusisha uchimbaji na ulazaji wa bomba za ukubwa wa inchi 8, 6, na 4 kwa umbali wa Kilomita 3.5, kazi ambayo hadi leo imefikia asilimia 95," amesema Mhandisi Jelson.
Jelson amesema mradi huu unaogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 237, utanufaisha zaidi ya wakazi 500 kwa kuwapatia huduma ya majisafi, salama na toshelevu kwa wakati wote huku akiwaondoa hofu wakazi wa Kinzudi kuwa hakuna ataerukwa katika kupatiwa huduma ya majisafi.
Kwa upande wake, Ndugu Iddy Nyamlani, mkazi wa mtaa wa Kinzudi ameipongeza DAWASA kwa kusikia na kutatua changamoto hii ya upungufu wa huduma katika mtaa wao na sasa wanaimami kubwa ya kuwa na huduma bora wakati wote.
"Tulikuwa hatuna uhakika wa huduma ya maji, yalikuwa yakitoka mara moja moja na hujui ni muda gani yatakatika, lakini kwa kazi hii kubwa tunayoishuhudia ambayo DAWASA wapo mbioni kuikamilisha, tunapata matumaini ya kuwa na huduma bora na endelevu ya maji wakati wote," ameeleza Ndugu Nyamlani.