Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA KINONDONI MTAA KWA MTAA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA
10 Oct, 2025
DAWASA KINONDONI MTAA KWA MTAA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Katika kuhitimisha wiki ya huduma kwa wateja inayoadhimishwa Oktoba 6-10 kila mwaka, Mkoa wa kihuduma DAWASA Kinondoni imewatembelea wateja, kusikiliza na kutatua changamoto za kihuduma kwa lengo la kuboresha huduma.

Meneja mkoa wa kihuduma DAWASA Kinondoni, Ndugu Tumaini Muhondwa amesema hizi ni jitihada za Mamlaka za kuwafikia wateja  karibu katika kuthamini nafasi yao pamoja na kutoa ushirikiano kwao.

"Tumewatembelea wateja wetu katika eneo letu la kihudum kwa lengo la kuwashukuru wateja kwa kuendelea kutuamini na tunaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha ili huduma ya maji iweze kuwafikia kwa ubora zaidi," amesema Ndugu Muhondwa.

Ndugu Muhondwa amesema katika kuwafikia wateja hao pia walifanikiwa kutoa elimu ya utunzaji wa miundombinu ya maji, ulipaji wa bili za Maji kwa wakati pamoja na kuwapatia elimu juu ya kutoa taarifa na kupunguza upotevu wa maji.

Wateja waliotembelewa ni pamoja na maeneo ya Mwananyamala, Kinondoni, Mikocheni, Msasani, Hananasifu na Kijitonyama. Wateja wakubwa waliotembelewa ni Sea Cliff Hotel, Tanzania Chamber of Commerce Zhe Jiang, Jangid, Airtel, Sheifee Hospital, Shoppers Plaza na US Embassy.

Ndugu Rukia Omary, Mkazi wa Hananasifu ameipongeza DAWASA kwa hatua waliofikia kuwatembelea wateja na kutoa elimu pamoja na kuwathamini nafasi yao na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha huduma ya maji inazidi kuboreshwa.

Wiki ya huduma kwa wateja mwaka 2025 imebeba kaulimbiu inayosema "Dhamira inayowezekana."