Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA KUBADILI TASWIRA YA USAFI KATIKATI YA DAR
22 Jul, 2026
DAWASA KUBADILI TASWIRA YA USAFI KATIKATI YA DAR

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa uondoshaji majitaka wa Buguruni, ambao umefikia asilimia 30 ya utekelezaji na unalenga kuboresha huduma za majitaka pamoja na usafi wa mazingira kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Msimamizi wa Mradi huo, Mhandisi Khalid Upunda, amesema kwa sasa kazi zinazoendelea ni pamoja na ufungaji wa mfumo wa umeme wa muda (Temporary Electric Panel) utakaowezesha shughuli za ujenzi wa mtambo wakati wakisubiri kukamilika kwa mfumo wa kudumu wa umeme.

Amesema pia ujenzi wa sakafu ya jengo litakalobeba mitambo ya uchakataji wa majitaka unaendelea, hatua ambayo ni muhimu kabla ya usimikaji wa mitambo hiyo. Aidha, ujenzi wa jengo la utawala unaendelea vizuri ili kuwezesha usimamizi na uendeshaji wa shughuli za mradi.

"Vilevile tunaendelea na uchimbaji wa takatope katika eneo litakalojengwa jengo la kutibu majitaka (Disinfection Building), ambalo ni sehemu muhimu ya hatua za mwisho za matibabu ya majitaka," amesema Mhandisi Upunda.

Mbali na kazi hizo, ujenzi wa mtambo wa kuchakata majitaka unaendelea sambamba na utekelezaji wa mtandao wa mabomba ya ukubwa wa inchi 28, 32 na 36 wenye urefu wa kilomita 16. Pia vituo vya kusukuma majitaka katika maeneo ya Jangwani na Gymkhana vinaendelea kujengwa.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mivinjeni, Fadiga Mtumwa, ameipongeza DAWASA kwa juhudi zake, akisema mradi huo utakuwa na mchango mkubwa katika kupunguza uchafuzi wa mazingira na magonjwa ya mlipuko yanayotokana na hali duni ya usafi.

"Mradi huu utasaidia kuboresha afya za wananchi na kuongeza mazingira safi kwa wakazi wa maeneo haya," amesema Mtumwa.

Mradi wa Usafi wa Mazingira wa Buguruni unagharimu Dola za Marekani milioni 70 na unatarajiwa kuhudumia wakazi 181,440. Wanufaika wakuu ni wakazi wa Manispaa ya Kinondoni katika maeneo ya Magomeni, Ndugumbi na Mzimuni, pamoja na wakazi wa Manispaa ya Ilala katika maeneo ya Mchikichini, Kariakoo, Jangwani, Gerezani, Kisutu, Mchafukoge, Upanga Mashariki, Upanga Magharibi na Kivukoni.