Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA, MANAWASA WABADILISHANA UZOEFU MAPAMBANO UPOTEVU WA MAJI
17 Sep, 2025
DAWASA, MANAWASA WABADILISHANA UZOEFU MAPAMBANO UPOTEVU WA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi Nachingwea (MANAWASA)Mtwara imevuna ujuzi wa namna bora ya kukabiliana na upotevu wa maji kutoka kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika kutoa tarifa za uvujaji. 

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya mafunzo iliyotanguliwa na kikao cha majadiliano ya kubaini changamoto za utoaji wa huduma ya maji kwa pande zote mbili, kwa lengo la kuboresha huduma. 

Akiwasilisha mikakati iliyopo na inayotekelezwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa upotevu wa maji imekuwa ni changamoto kubwa katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam, lakini kwa kuwashirikisha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wenye mawasiliano katika makazi ya wananchi. 

Amesema kuwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni nyenzo muhimu kwa kuwa wanasaidia kutoka taarifa za mara kwa mara za uvujaji wa maji kwenye maeneo ya wananchi. 

Mbali na hapo, Mamlaka imebuni teknolojia ya kisasa ya namna ya kukabiliana nayo ikiwemo matumizi ya scada kwa lengo la kubaini kiasi cha maji kinachozalishwa na yanayouzwa ili kupata mapato ya Serikali na kukidhi gharama za uendeshaji. 

Mhandisi Bwire amesema kuwa kupitia mfumo wa scada ambao umeanza kufungwa katika maeneo ya Kinondoni, Mlandizi na Mkuranga kama majaribio, Mamlaka imeweza kubaini kiasi cha maji kinachozalishwa na kiasi kinachotumika na kubaini maji yanayopotea bila kulipiwa. 

"Kwa sasa teknolojia hii imeanza kuleta matokeo chanya kwa kuanza kupunguza kiwango cha upotevu wa maji katika maeneo inayotumika kutoka asilimia 50 mpaka asilimia 35," amesema Mhandisi Bwire. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MANAWASA Ndugu Kiula Kingu ameipongeza DAWASA kwa jitihada kubwa wanazochukua za kukabiliana na upotevu wa maji. 

Ameongeza kuwa kwa upande wa MANAWASA upotevu wa maji kwa sasa ni asilimia 19 hadi 21, na lengo ni kupunguza na kukomesha kabisa upotevu, na kazi inaendelea ya kushirikisha wananchi kutambua umuhimu wa kuzuia upotevu wa maji. 

Amesema kuwa kazi inaendelea ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika ulinzi wa miundombinu ya maji sambamba na kukabiliana na uvujaji wa maji katika maeneo yao. 

Pia ameishukuru DAWASA kwa kuwashirikisha mkakati wa namna ya kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa kuongeza maunganisho ya maji kwa wananchi.