DAWASA, MBUNGE SEGEREA WAJADILI UBORESHAJI HUDUMA ZA MAJI BONYOKWA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imefanya kikao kazi na Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mheshimiwa, Agnesta Kaiza.
Kikao hicho ambacho kimeshirikisha Wenyeviti wa Mitaa ya Bonyokwa, Kisiwani na Msingwa yenye wakazi takribani 26,516 ndani ya Kata ya Bonyokwa kilikuwa na lengo la kuboresha huduma ya majisafi ndani ya kata hiyo.
Katika kikao hicho, taarifa za maeneo yenye changamoto zimewasilishwa, ikiwa ni pamoja na mitaa yenye uhaba mkubwa wa maji na uhitaji wa upanuzi wa miundombinu sambamba na kikao hicho, Mbunge pamoja na watendaji wa DAWASA wamefanya ziara ya kutembelea na kukagua maeneo yenye changamoto kubwa zaidi ili kuona hali halisi na kuwezesha kuweka vipaumbele vya kuboresha utoaji wa huduma.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Segerea, Mheshimiwa Agnesta Kaiza amesema DAWASA inapaswa kuboresha huduma ya majisafi katika eneo la Bonyokwa kwani ni katika maeneo korofi ambayo yanapata maji Kwa mgao na msukumo mdogo kutokana na jiografia ya miinuko mikali.
“Wananchi wetu wanastahili kupata huduma ya maji Kwa uhakika, changamoto tulizozipokea leo ni muhimu sana, na naamini kwa ushirikiano wa karibu kati yetu na DAWASA," amesema Mheshimiwa Agnesta.
Mheshimiwa Agnesta ametoa wito kwa watendaji wa DAWASA kufika katika mitaa ili kutatua changamoto zozote zinazojitokeza ili kila mwananchi anufaike na uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Kwa upande wake, Meneja wa mkoa wa kihuduma DAWASA Tabata, Ndugu Gilbert Massawe amesema dhamira ya ziara hiyo ni kusikiliza wananchi kwa kushirikiana na viongozi wakiongozwa na Mbunge ili kupata suluhu ya haraka ya kuboresha huduma ya majisafi kwa wakazi wa kata ya Bonyokwa.
“Tumeanza kwa kuboresha uhusiano na viongozi ili kurahisisha utoaji wa taarifa lakini pia kuongeza usimamizi katika usambazaji maji pamoja na kuboresha miundombinu chakavu Kwa lengo la kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa maji," amesema Ndugu Massawe.
