Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MAMLAKA YAWEKA MSISITIZO MATUMIZI SAHIHI MIFUMO YA MAJITAKA
25 Feb, 2026
MAMLAKA YAWEKA MSISITIZO MATUMIZI SAHIHI MIFUMO YA MAJITAKA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na zoezi la usafishaji na uimarishaji mifumo ya majitaka sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam.

Zoezi hilo linalenga ufanisi katika mifumo hiyo na kuzuia uzibaji wa mara kwa mara unaosababisha uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha afya ya jamii.

Akizungumzia zoezi hilo, Mhandisi Mbaraka Mpala amesema Mamlaka inataratibu ya kuikagua mifumo ya majitaka na kuisafisha mifumo hiyo mara kwa mara ili kuepuka changamoto ya utiririshaji majitaka mitaani.

"Tunapitia mifumo hii mara kwa mara, lengo ni kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi, shughuli zinazofanyika ni pamoja na usafishaji wa chemba ambapo tunaondoa taka zilizopo kuruhusu mfumo kufanya kazi kwa ufanisi.

Pia, ujenzi wa mifuniko ya chemba unaendelea ili kuhakikisha hakuna chemba inayobaki wazi kuingiza taka katika mfumo pamoja na kuhatarisha maisha ya wananchi," amesema Mhandisi Mpala.

Mpala amewahasa wananchi kuwa na matumizi sahihi ya mifumo ya majitaka kwa kuacha kutupa taka ngumu kama mifuko ya plastiki, matairi, nguo na mawe zinazopelekea mifumo hiyo kuziba mara kwa mara.

"Lakini pia sehemu mbalimbali tumepata changamoto ya mifuniko ya chemba za majitaka kuibiwa, chemba hizo zinapobaki wazi huingiza taka ngumu na wengine hutumia kama sehemu ya kuhifadhi uchafu.

Mbali na hilo, chemba zinapobaki wazi huatarisha maisha ya wapita njia, hivyo yeyote atakayebainika kuhujumu miundombinu hii ya majitaka atachukuliwa hatua za kisheria" amesema Mpala.

Ndugu Abdala Ally, Mkazi wa Mwenge ameshukuru DAWASA kuchukua hatua za haraka pale wanapowapatia taarifa ya utiririshaji wa majitaka unaosababishwa na mifumo kutofanya kazi vizuri kwani hufika kwa wakati na kutatua changamoto hiyo, hali inayofanya Mazingira yetu yaendelee kuwa safi na salama.