Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA, MORUWASA WABADILISHANA UZOEFU USIMAMIZI RASILIMALI MAJI
09 May, 2025
DAWASA, MORUWASA WABADILISHANA UZOEFU USIMAMIZI RASILIMALI MAJI

Viongozi waandamizi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wametembelea Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) kwa lengo la kujenga na kubadilishana uzoefu katika usimamizi rasilimali Maji.

Katika ziara hiyo vuongozi hao wamejadili na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yakiwemo uimarishaji huduma za maji kwa Wananchi, mapambano ya upotevu maji na namna bora ya kuimarisha Mawasiliano baina ya Mamlaka hizo.

Aidha, Viongozi hao wamepata nafasi ya kutembelea Bwawa la Mindu lililopo Kata ya Mindu, Manispaa ya Morogoro ambalo ni moja ya chanzo cha maji linalopeleka maji katika Mtambo wa Uzalishaji Maji Mafiga ulio na uwezo wa kuzalisha lita Milioni 27 kwa siku na kuhudumia asilimia 75 ya wateja wa Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA, Ndugu Lyang'onjo Kiguhe ameipongeza DAWASA kwa kufanya ziara hiyo katika Mkoa na Mamlaka yao kwani ni hatua ya kufahamiana zaidi na kujenga Mahusiano ya kihuduma.

“MORUWASA tumefurahi na tunashukuru kwa kutembelewa na DAWASA kwa lengo la kuimarisha uhusiano wetu, kupitia ziara hii na ukubwa wa DAWASA tumejifunza mengi na tunaamini yametujenga katika kuboresha huduma kwa wananchi tunaowahudimia” alisema Kiguho. 

Meneja wa Rasilimali Watu DAWASA, Bernadeta Mwabusila ameipongeza MORUWASA kwa ushirikiano mzuri na kuahidi kuendelea kuimarisha mahusiano ya utendaji kazi.

"Watumishi wa Umma tunahitaji kuwa na ushirikiano mzuri ili kuinua tija mahala pa kazi na kwa kupitia ziara hii, DAWASA na MORUWASA tumeweza kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na kuwezesha watumishi hawa kuimarisha Sekta muhimu ya maji” amesema Mwabusila.