Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA MTAANI KUHAMASISHA ULIPAJI WA BILI ZA MAJI
25 Apr, 2025
DAWASA MTAANI KUHAMASISHA ULIPAJI WA BILI ZA MAJI

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na zoezi la kutembelea wateja katika mitaa mbalimbali ya maeneo ya Kihuduma ili kuhamasisha ulipaji wa bili za maji kwa wakati.

Akielezea lengo la zoezi hilo, Afisa Biashara wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Ukonga, Bw. Andrew Goodluck Mtenga amesema kuwa Mamlaka inaendelea na zoezi maalum la kupita nyumba hadi nyumba na Mtaa kwa Mtaa ili kutoa elimu na kufuatilia wateja wenye madeni ya huduma.

"DAWASA tunaendelea na zoezi la kuwatembelea wateja katika maeneo ya Mitaa ya Pugu, Gongolamboto, Kisumu na Ulongoni kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu huduma, kuwahamasisha ulipaji wa bili za maji kwa wakati pamoja na kuhakikisha wateja hawabaki na malimbilizo ya madeni ya bili za miezi ya nyuma," ameeleza Bw. Mtenga.

Aidha, Bw. Mtenga, ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa za mivujo au uharibifu wa miundombinu ya maji kupitia mawasiliano ya huduma kwa wateja.

Naye Mkazi wa Pugu Kisumu Bi. Tatu Kazumari ameipongeza DAWASA kwa kuwa karibu na wateja na kufuatilia madeni ili kupunguza malimbilizo ambayo yanaweza kuathiri upatikanaji wa huduma za maji endapo hayatolipwa kwa wakati.

"Hatua ya DAWASA kututembelea mara kwa mara inatusaidia kutukumbusha kulipa bili zetu kwa wakati na kuepuka madeni kuwa makubwa ambayo hatimaye tunaweza kusitishiwa huduma pasipo kutarajia, zoezi hili liwe endelevu ili tuwe tunahamasika na pia kutusaidia tunapokuwa na changamoto mbalimbali za huduma ya maji," amesema Bi. Tatu.

Kwa upande wake Bw. Ramadhan Suleyman Mngweme, Mkazi wa Ulongoni B' amesema kuwa  wanashirikiana vizuri na wasomaji mita na kupata msaada pale anapohitaji.

"Kwa kweli huduma ya maji tunapata vizuri, wanasoma mita kwa wakati na tunapata bili kama nilivyotumia na kwa wakati. Huduma ya maji ni yetu, tujiunge, tutumie na tuzingatie kulipa bili kwa wakati," amesema Bw. Mngweme.

DAWASA inaendelea na zoezi la ufuatiliaji wa madeni ya maji katika maeneo yote ya Kihuduma na kuwasisitiza wateja kulipa bil kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa maji.