DAWASA NA BODABODA KUSHIRIKIANA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekutana na kutoa elimu kwa vikundi vya watoa huduma ya usafiri maarufu kama wa Bodaboda kwa lengo la kujenga ushirikiano katika ulinzi wa miundombinu ya maji na utoaji wa taarifa za upotevu wa maji katika eneo la kihuduma la DAWASA
Mamlaka imekutana na wadau hawa katika maeneo ya Kisarawe, Mkuranga, Kigamboni, Kawe, Magomeni, Kinondoni, Mabwepande na Bagamoyo na zoezi linaendelea katika maeneo mengine ili kujenga mahusiano ya kiutendaji kati ya DAWASA na vikundi hivyo katika jamii.
Afisa Uhusiano DAWASA, Jamal Chuma amesema lengo la DAWASA kuwatembelea watoa huduma hao ni kuwatambua kama wadau muhimu katika utoaji huduma ya Maji na kuwasihi kutoa taarifa za mivujo na upotevu wa Maji katika maeneo yao ya kazi.
“Kundi hili ni muhimu sana kwani muda mwingi wanatembea katika maeneo mengi katika mitaa ambayo nasi DAWASA tunatoa huduma mchana na usiku. Tumewaomba wawe mabalozi wazuri katika kutoa taarifa za mivujo ya Maji kwa kutoa taarifa kwenye Mamlaka ili zifanyiwe kazi” alisema ndugu Chuma
“Tumewapa elimu jinsi ya kutambua uvujaji wa maji ya DAWASA na mahali sahihi pa kuwasilisha taarifa hizo katika kituo cha huduma kwa wateja pamoja na namba za simu za Mikoa ya kihuduma kwa urahisi wa kuzishughulikia kwa wakati ili kwa pamoja tuokoe maji yanayopotea na kuhakikisha huduma inafika kwa kila Mwananchi” alisisitiza Chuma
Nae Ndugu, Khalfani Hamisi boda boda kutoka Kigamboni ameipongeza DAWASA kwa kuwatembelea na kutoa elimu hiyo kwani itasaidia kuzuia upotevu wa maji ambayo ni hasara kwa Serikali na Jamii pia.
"Elimu hii ni ya muhimu kwani huwa mtaani tunakutana na mivujo mingi katika maeneo tunayotoa huduma na pia namba za mawasiliano za DAWASA tulizopatiwa zitatusaidia kureport na hivyo kuondoa mivujo ya maji. Tunaahidi kushirikiana na DAWASA bega kwa bega" alisema Ndugu Khalfani