Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA NA VIONGOZI KATA KAWE WAAINISHA MIKAKATI KUBORESHA HUDUMA YA MAJI
09 Dec, 2024
DAWASA NA VIONGOZI KATA KAWE WAAINISHA MIKAKATI KUBORESHA HUDUMA YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imefanya kikao na viongozi wa kata ya Kawe inayohudumiwa na Mkoa wa DAWASA Kawe kwa lengo la kuweka mikakati ya uboreshaji huduma za maji itakayosaidia kupunguza changamoto kwa Wananchi. Kikao kazi hicho kilichohusisha Maafisa kata, Watendaji na Wenyeviti wa Serikali za mitaa.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Kawe Mhe. Rehema Msuta ameipongeza Mamlaka kwa kuendelea kuwa karibu na wadau muhimu katika kuimarisha huduma akitoa rai kwa ofisi ya Mkoa wa kihuduma DAWASA kawe kuendeleza ushirikiano na viongozi ngazi ya Kata na Serikali za mtaa ili kutatua changamoto mbalimbali za Wananchi kwa wakati 

“Naipongeza DAWASA kwa kuendelea kushirikisha katika mipango na mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi kwani hii inatusaidia kupata taarifa sahihi za taratibu mbalimbali katika kujibu hoja za wananchi” Amesema Mhe. Rehema 

Naye mwakilishi wa Mtendaji Kata ya Kawe, ndugu Esther Mwamyalla ameongeza kwa kuiomba Mamlaka kuongeza jitihada za kushughulikia taarifa za mivujo katika mitaa, na kutoa rai kwa wafanyakazi wa DAWASA kujenga uzalendo ili kuongeza uwajibikaji kwa wananchi. 

“Mamlaka imekuwa ikifanya kazi kubwa kushughulikia malalamiko mbalimbali kwa hilo niwapongeze japo kuna mahali pa kuongeza juhudi zinapotolewa taarifa za mivujo zinapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka, hili liwe jukumu kwa watu wafanyakazi wote na sio mafundi tu” amesema Mhe. Esther Mwamyalla 

Meneja wa DAWASA Kawe, Ndugu Haruna Taratibu ameelezea hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi katika kata ya Kawe kuwa ni nzuri na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano na viongozi wa kata katika kutoa huduma pamoja na changamoto mbalimbali zinazoukuta Mkoa kama vile malimbikizo ya madeni ya maji pamoja na ulinzi wa mindombinu ya maji kwa baadhi ya maeneo. 

“Mamlaka inajitahidi kukabiliana na hali ya upungufu wa huduma ya maji hivyo tunawasihi wateja kukumbuka kuwa na vyombo vya kutosha kuhifadhi maji ili kuepuka usumbufu wa kukosa maji pale huduma inapokosekana”  Amesema Ndugu Taratibu