DAWASA NYUMBA KWA NYUMBA MAUNGANISHO MAPYA YA WATEJA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mkoa wa Kihuduma Tegeta imeendelea na maunganisho ya wateja wapya kwa kuwafikishia wateja vifaa vya maunganisho mapya majumbani.
Sambamba na kufikishiwa vifaa vya maunganisho majumbani, watumishi wa Mamlaka walitoa elimu ya utunzaji miundombinu ya majisafi na ulipaji wa ankara kwa wateja.
Akizungumzia zoezi hilo, Mhandisi Dominick Mkamba amesema Mamlaka imemsogezea huduma mwananchi kwa kupelekewa vifaa vyake vya maunganisho majumbani jambo ambalo litaokoa muda na gharama kwa wateja na kuendelea na shughuli nyingine.
"Mteja ataletewa vifaa nyumbani na utaratibu wa kumuunganishia maji utaanza, wateja waliolipia maunganisho ya maji wote watapa huduma hii.
Tumedhamiria kumuondolea usumbufu na gharama mteja wa kufata vifaa ofisini, niwahakikishie wateja wetu kila atakaeomba huduma ya maji, tutampatia huduma hiyo kwa haraka," amesema Mhandisi Mkamba
Amesema jumla ya kaya 30, kutoka maeneo ya Mtongani, Salasala na Tegeta Nyuki wamefikishiwa vifaa vyao majumbani na sasa wanakwenda kupata huduma bora ya majisafi na yenye gharama nafuu.
Kwa upande wake, Ndugu Lazaro Michael, Mkazi wa Mtongani amesema amefurahishwa na wepesi wa DAWASA kumfikishia huduma ya maji nyumbani kwake na sasa mambo mengi yaliyokwama kutokana na ukosefu wa maji yataendelea tena.
"Tuwapongeze DAWASA kwa kutufikishia huduma ya maji mtaani kwetu, binafsi imechukua muda mfupi toka nilipoomba na sasa wameniletea vifaa hivi nyumbani kumaanisha huduma ya maji ni rasmi nakwenda kuipata," amesema Ndugu Lazaro.
