UJENZI KITUO CHA KUSUKUMA MAJI GOLANI WAFIKIA ASILIMIA 80, WAONGEZA KICHEKO GOLANI, SARANGA NA UKOMBOZI
Wakazi wa Mtaa wa Golani, Kata ya Kimara, Wilaya ya Ubungo wafurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (booster pump) katika eneo hilo uliofika asilimia 80 za ukamilishwaji wake na unaotajwa kwenda kihudumia wakazi takriban 5,000 wa eneo la Golani, Ukombozi pamoja na Saranga.
Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa gharama za shilingi milioni 291 na unatarajia kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji eneo la Golani pamoja na maeneo ya jirani.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Golani, Ndugu Gabriel Kilave amesema kwa sasa wananchi wa eneo hilo wamekuwa na matumaini makubwa baada ya kujionea kwa ukaribu kazi kubwa inayoendelea ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na ushirikiano wa majibu ya haraka yanayotolewa na DAWASA kuhusu ukamilikaji wake.
"Tunafurahishwa na kasi ya utekelezwaji wa mradi huu DAWASA wanaupiga mwingi sana, maana tunaimani sasa tutaanza kutumia maji kwa gharama ndogo kuliko sasa. Tumeambiwa mradi upo mbioni kikamilika na tumeona umefikia asilimia 80 kitu ambacho kinatia moyo na kuongeza furaha kwenye nyuso zetu," amesema Kilave.
Kwa upande wake mkazi, mkazi wa Golani, Ndugu Sauda Rashid, amesema wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya ukosefu wa maji kwa kipindi kirefu sana na sasa kupitia mradi huu adha hiyo inakwenda kufutika moja kwa moja.
"Naipongeza DAWASA kwa kasi waliyoitumia kuhakikisha wanaenda kukamilisha utekelezaji wa mradi kama walivyoahidi, tunafahamu mradi ungewahi kukamilika zaidi ila changamoto za hali ya hewa kwa maana mvua zimepunguza kasi lakini bila hivyo sasa hivi tungekuwa tunaogelea kwa maji ya DAWASA" amesema Sauda.
Naye msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Fadhili Mndeme amewahakikishia wakazi wa Golani mradi unaendelea vizuri katika utekelezaji wake na Mamlaka inahakikisha ifikapo mwisho wa mwezi Mei 2026 mradi utakuwa umekamilika na kuanza kutoa huduma.
Sanjali na hayo, Mhandisi Mndeme amesema kazi iliyobaki kwa sasa ni kukamilisha ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (pump house), kufunga pampu pamoja na kuunganisha mfumo wa umeme (transfoma) zitakazoweza kusukuma lita laki 1.5 za maji kwa saa, na kunufaisha wakazi takribani 5,000 wa maeneo ya Golani, Saranga, Ukombozi, Mnazi Mmoja pamoja na Mnara wa Voda.
