Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA, WADAU WAJIFUNGIA KUJADILI USAFI WA MAZINGIRA
07 Aug, 2025
DAWASA, WADAU WAJIFUNGIA KUJADILI USAFI WA MAZINGIRA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya usafi wa mazingira kujadiliana kwa pamoja jinsi ya kuhamasisha uboreshaji wa usafi wa mazingira katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo yaliyo nje ya mtandao.

Akifungua mafunzo hayo, Msimamizi wa miradi wa DAWASA, Mhandisi Fredrick Mujungu amesema mafunzo haya ni sehemu ya jitihada za mamlaka kuimarisha usafi wa mazingira kupitia ushirikiano wa karibu na wadau muhimu huku elimu kwa umma ikiwa ni nguzo kuu ya mafanikio.

“Lengo kuu la mkutano huu ni kutoa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kudumisha usafi wa mazingira, matumizi sahihi ya miundombinu ya maji na majitaka, pamoja na kujadili changamoto zinazokwamisha juhudi za pamoja katika sekta hii muhimu,” amesema Mhandisi Mujungu.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka kampuni ya kishauri ya Economic Business Foundation Sanitation Marketing Consultant (EBF), Leonard Sibomana amesema mafunzo haya yataimarisha ushirikiano wa karibu na wadau muhimu pamoja na kuimarisha mahusiano na watoa huduma binafsi katika kuboresha huduma za usafi wa mazingira.

“Changamoto za usafi wa mazingira haziwezi kutatuliwa na mamlaka peke yake. Tunahitaji mshikamano wa pamoja kati ya sekta binafsi, jamii na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha maeneo yetu yanakuwa safi, salama na yenye mazingira rafiki kwa afya ya binadamu,” amesema Sibomana.

Naye Katibu wa watoa huduma binafsi wa usafi wa mazingira, Hamis Juma ameipongeza DAWASA kwa kuchukua hatua hiyo ya kuwaleta pamoja na kutoa elimu na kusisitiza mafunzo ya aina hiyo yanapaswa kuwa endelevu na kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii, hususan vijana na wanawake.

Katika mafunzo haya, mada mbalimbali ziliwasilishwa na wataalamu wa afya na mazingira, wakisisitiza umuhimu wa matumizi salama ya vyoo, uondoshaji wa taka ngumu na majitaka, pamoja na athari za uchafuzi wa mazingira kwa afya ya jamii.