DAWASA YAANZA MWAKA NA WAKAZI WA GEZAULOLE

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imepeleka furaha ya mwaka mpya 2025 kwa kuanza kutekeleza mradi wa Maji katika kata ya Gezaulole Wilayani Kigamboni utakaohudumia Wakazi takribani 7200 katika mitaa ya Kizani, Kibugumo, Mwela, Mbwa-Maji, Gezaulole na Kigogo
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni ambaye ni Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni Bi. Loyce Mwasaga ameshuhudia upokeaji wa miundombinu hiyo na kuipongeza DAWASA kwa jitihada zilichokuliwa kwa haraka na kasi za kuhakikisha inasogeza huduma ya maji Kigamboni.
"Kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni niwapongeze DAWASA kwa kuanza utekelezaji wa mradi huu ambapo kwa siku ya leo tumeshuhudia mabomba takribani 5,000 yamefikishwa hapa ili kazi ya kuunganishia wateja ianze mara moja." amesema Bi. Mwasaga
Msimamizi wa mradi kutoka DAWASA Mhandisi Jerryson Kazungu amesema utekelezaji wa mradi huo utahusisha ulazaji wa bomba za inchi 12 kwa umbali wa kilomita 20 ndani ya Kata ya Gezaulole katika mitaa saba iliyobakia bila huduma ya Maji ya DAWASA.
"Tukikamilisha mradi huu, mitaa iliyokuwa haina huduma katika Kata ya Gezaulole sasa itaondokana na adha ya maji kupitia mradi huu wenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.3“ amesema Mhandisi Kazungu.