DAWASA YAASA WATEJA UHAKIKI WA USOMAJI DIRA ZA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa kihuduma Mabwepande umeendelea kuwakumbusha wateja juu ya umuhimu wa usomaji na uhakiki mita pindi wanapo pokea ujumbe wa usomaji kwenye simu zao ili kuongeza uwazi na ufanisi katika usimamizi wa utoaji huduma.
Akizungumza, Afisa Biashara wa DAWASA Mabwepande, Ndugu Rajab Mpinzire amesema zoezi la usomaji mita kwa kushirikiana na wateja linaendelea sambamba na uhakiki wa usomaji ambapo wateja wanapata nafasi ya kuhakiki mita zao kabla ya kuandaliwa bili za mwezi.
"Zoezi la usomaji mita bado linaendelea na baadhi ya wateja tayari wameshapokea jumbe fupi za uhakiki wa usomaji, tunatoa rai kwa wateja wetu kuwa ni muhimu kuhakiki usomaji mita na kutoa taarifa kama kuna changamoto ili tuifikie kwa wakati.
Taarifa hizo zinapokelewa kupitia namba za huduma kwa Wateja 181 (bure), Mitandao ya kijamii au wafike katika ofisi zetu kwa msaada zaidi," amesema Ndugu Mpinzire.
Ndugu Mpinzire amesisitiza ushirikiano kati ya wateja na Mamlaka ni muhimu hivyo anaendelea kuwasihi wateja kutoa ushirikiano kwa watumishi pindi wanapopita katika makazi yao.
Mkoa wa kihuduma DAWASA Mabwepande una jumla ya wateja takribani 20,662 na unahudumia Kata za Bunju na Mabwepande.
