DAWASA YABORESHA HUDUMA YA MAJI VETA - AIRPORT

Kazi ya kukagua miundombinu ya usambazaji maji pamoja na kupima msukumo wa maji katika eneo la Veta, ikiwa imetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika eneo la Viwanda vilivyopo ukanda wa barabara ya Nyerere.
Mhandisi John Asenga kutoka Idara ya Uzalishaji na Usambazaji Maji amesema kuwa kazi hiyo ni utekelezaji wa agizo la Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire kufuatia ziara ya kukagua hali ya upatikanaji maji eneo la Temeke mnamo tarehe 12.11.2024.
"Zoezi hili linajumuisha kukagua mfumo wetu wa usambazaji maji pamoja na kupima msukumo wa Maji kwa lengo la kuhakikisha wateja wetu waliopo ukanda huu wa Barabara ya Nyerere wanapata huduma ya uhakika. Kazi hii inategemea kukamilika ndani ya muda wa wiki mbili kuanzia sasa," amesema.