DAWASA YACHOCHEA UTALII MSITU WA PUGU-KAZIMZUMBWI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imetekeleza mradi wa Maji wenye thamani ya Shilingi Milioni 16.11 kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika eneo la Kinyanyiko ndani ya msitu wa Kazimzumbwi, Kata ya Kisarawe, Wilaya ya Kisarawe unaotajwa kwenda kuchochea kasi ya utalii katika Mkoa wa Pwani.
Mradi huo unahusisha uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya inchi 3 hadi inchi 1.5 kwa umbali wa kilometa 12 ndani ya msitu ili kufikisha huduma ya maji katika ofisi ya kituo cha Utalii wa ndani (Ushoroba wa Pugu-Kazimzumbwi) ambapo kukamilika kwa maunganisho ya upatikanaji wa huduma hiyo kutachochea Utalii kwa zaidi ya watu 1,500 wanaotembelea katika kituo hicho kila mwezi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhandisi Ermina Audiphas wa Mkoa wa Kihuduma Kisarawe amesema "Mradi huu umeanzia eneo la Minaki shuleni hadi eneo la Kinyanyiko kwenye eneo la uwekezaji na mradi umeshakamilika na hivi karibuni mteja ataanza kutumia maji kwa manufaa yake na wageni watakaotembelea kituo hicho." Ameeleza Mha. Ermina.
Kwa upande wake, Meneja wa TFS Wilaya ya Kisarawe Baraka Abraham Mtewa ameishukuru DAWASA kwa kuwawekea huduma ya maji katika eneo hilo la kituo cha uwekezaji ambapo patakuwa na eneo la kutazama jiji (view point), mgahawa wa chakula, bwawa la kuogelea na kiwanja cha michezo ambapo vyote hivyo vinahitaji sana huduma ya maji hivyo itachochea kasi ya utalii katika kituo hicho.