DAWASA YAENDELEA KUBORESHA UFANISI WA DIRA ZA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na zoezi la kusafisha dira (mita) za maji kwa wateja zenye changamoto mbalimbali ikiwa ni sehemu ya hatua madhubuti zenye lengo la kuboresha ufanisi wa mita hizo.
Akizungumzia zoezi hilo, Afisa Ankara wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma wa Kisarawe, Ndugu Allan Majebele amesema kuwa kazi ya usafishaji mita inaendelea kutekelezwa katika maeneo ya Umatumbini, Ngugu, Sanze, Pugu, Bane, Kisarawe mjini na eneo lote la kihuduma kwa wateja wote ambao mita zao hazisomeki vizuri au zimepungua ufanisi wake.
"Lengo la zoezi hili endelevu ni kuongeza ufanisi wa mita hususan zile zenye ukungu na chembechembe za mchanga au uchafu ulionasa katika chujio la mita ili kusaidia kuzuia upotevu wa maji, mita kusomeka kwa ufasaha pamoja na kurahisisha uhakiki wa usomaji kabla ya bili za kila mwezi kutolewa kwa wateja". Ameeleza Majebele.
Mamlaka inaendelea kuwasisitiza wateja wote kutoa ushirikiano kwa watumishi wa DAWASA wakati wa zoezi la usafishaji mita pamoja na usomaji mita shirikishi linalofanyika kila mwezi. Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia kituo cha huduma kwa wateja 0800110064 (bure) au
0735 202 121(WhatsApp tu).