DAWASA YAIBUA TABASAMU KWA WAKAZI WA BAGAMOYO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeibua na kuamsha tabasamu kwa wakazi takriban 70 wa wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani baada ya kuwapatia vifaa vya maunganisho ya huduma ya maji safi kupitia Mkoa wa Kihuduma wa DAWASA Bagamoyo.
Akizungumza wakati wa zoezi la maunganisho ya wateja wapya wa maji katika Mkoa huo wa kihuduma, Mhandisi wa Miradi wa DAWASA Bagamoyo Bw. Mohammed Ahmad amesema "Zoezi hili limehisusisha utoaji wa vifaa vya maunganisho ya huduma ya majisafi kwa wateja wapatao 70 ambao ni miongoni mwa waliokamilisha kulipia huduma hiyo kwa kipindi kilichopita na sasa wamepata fursa ya kupatiwa vifaa hivyo tayari kuunganishwa na huduma waliyokuwa wanaisubiri kwa hamu kubwa".
Mhandisi Ahmad ameongeza kuwa lengo la kutoa vifaa hivyo kwa wateja hao ni kuwaunganishia na kusogeza huduma kwa wananchi wa kata za Zinga, Bagamoyo Mjini, Kilomo na Yombo pamoja na kuhakikisha wananchi wote wa Bagamoyo wanapata huduma ya majisafi na salama.
Kwa upande wake mwananchi wa Kata ya Zinga Mpya, Bw. Riziki Enock Mandazi amesema "Leo nina furaha na ninashukuru nimepatiwa vifaa vyangu na DAWASA kwa ajili ya kunganishiwa huduma ya maji na natumaini kuanzia sasa naenda naenda kufurahia huduma ya maji nyumbani kwangu". Ameeleza Mandazi.
Naye mkazi wa Kata ya Bagamoyo, Bi. Rozina Bernad amesema "Tunaishukuru sana DAWASA, tumesubiri kwa muda mrefu, leo tumepata maji tumefurahi, tutaoga na kupika kwa maji mazuri, shukrani sana kwa DAWASA". Ameeleza Bi. Rozina.
Zoezi hili la ugawaji wa vifaa vya maunganisho limeambatana na utoaji wa elimu ya utunzaji miundombinu ya maji, usomaji wa mita na uhakiki kabla ya bili kutolewa, umuhimu wa kulipa bili kwa wakati na utoaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo zinazohusu uvujaji, uharibifu wa miundombinu na nyinginezo.