Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAIMARISHA HUDUMA MAKANGARAWE KUPITIA NISHATI YA JUA
16 Apr, 2026
DAWASA YAIMARISHA HUDUMA MAKANGARAWE KUPITIA NISHATI YA JUA

Wakazi wa Mtaa wa Makangarawe, Kata ya Makangarawe, Wilaya ya Temeke, wanatarajia kunufaika na huduma ya majisafi na salama kwa saa 24 kufuatia utekelezaji wa mradi wa kisima cha maji unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Mradi huo wenye thamani ya Shilingi Milioni 190 unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu chenye kina cha mita 12 unatarajiwa kuzalisha takribani lita 240,000 za maji kwa siku, kiasi kitakachowanufaisha zaidi ya wakazi 2,000 wa Kata ya Makangarawe.

Akizungumza wakati wa Mwenge wa Uhuru kitaifa na uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi huo, Msimamizi wa mradi , Mhandisi Aziz Namanga, alieleza kuwa mradi umewekewa mfumo wa nishati ya jua ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji hata pale umeme wa kawaida unapokatika.

“Mradi huu umewekewa mfumo wa umeme wa jua (solar) wenye uwezo wa kilowati 17.15, hivyo huduma ya maji itaendelea kupatikana wakati wote, hata wakati wa mgao au hitilafu za umeme wa kawaida. Hii inahakikisha wananchi wanapata maji kwa uhakika,” amesema Mhandisi Namanga.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ndugu Wazo Mwang'onda, alieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi akibainisha kuwa utawanufaisha wananchi wengi, hususan wale ambao bado hawajafikiwa na mtandao wa maji majumbani.

“Mwenge wa Uhuru umefika katika mradi huu, umepokea taarifa na kuukagua, na tumeridhishwa na maendeleo yake. Maji tayari yanatoka, na ujenzi unaendelea ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa. Kwa wale ambao mtandao wa maji haujafika majumbani, wamefungiwa mabomba hapa kisimani ili waweze kuchota maji kwa gharama nafuu,” amesema Mwang'onda.