DAWASA SASA RASMI MSUMI. WAKAZI 300 KUUNGANISHIWA HUDUMA
Wakazi wa eneo la Msumi, Kata ya Mbezi wilayani Ubungo, wameanza kupata huduma ya majisafi kufuatia kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Msumi uliotekelezwa na DAWASA kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 1.2.
Kupitia mradi huo, wakazi wameanza kukabidhiwa vifaa vya maunganisho mapya sambamba na kuunganishiwa huduma ya maji moja kwa moja kwenye makazi yao, hatua iliyopokelewa kwa furaha kubwa na wananchi wa eneo hilo.
Zoezi hilo linafanywa na watendaji wa DAWASA kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaanza kupata huduma ya maji safi kwa urahisi na kwa wakati.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa vifaa hivyo, Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA Ubungo, Mhandisi Alphonce Magoma, amesema tayari wakazi takribani 300 wamekabidhiwa vifaa vya maunganisho baada ya kukamilisha malipo ya huduma hiyo.
“Baada ya kukamilika kwa mradi wa Msumi, tayari pampu imeanza kufanya kazi na wananchi wameanza kupata maji. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi anayehitaji huduma anapata kwa wakati,” amesema Magoma.
Ameongeza kuwa zoezi la maunganisho linaendelea, huku DAWASA ikitarajia kuunganisha zaidi ya wateja 47,500 katika maeneo ya Msumi A, Msumi B, Msumi C pamoja na maeneo ya jirani.
Kwa mujibu wa Magoma, mamlaka hiyo pia imejipanga kuweka dawati maalumu la siku saba ili kuhakikisha wananchi wote wanaomaliza taratibu zao wanaunganishiwa huduma kwa haraka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Msumi, Jaqueline Juma, ameipongeza DAWASA kwa kutekeleza ahadi yake ya kupeleka maji katika eneo hilo, akisema mradi huo umeondoa changamoto kubwa iliyokuwa ikiwasumbua wananchi kwa muda mrefu.
“Wananchi wa Msumi tuna furaha kubwa sana. Walituahidi maji na kweli wametekeleza. Sasa Msumi kumenoga tofauti na zamani,” amesema Jaqueline.
Naye mkazi wa eneo hilo, Salome Rashid, amesema ujio wa huduma hiyo utarahisisha maisha ya wananchi wengi waliokuwa wakikabiliwa na adha ya kutafuta maji kwa muda mrefu.
Mradi wa Maji wa Msumi unatajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
