DAWASA YAIMARISHA HUDUMA YA MAJISAFI MIHANDE
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Mlandizi, umekamilisha kazi ya matengenezo ya miundombinu ya bomba na huduma kurejea kama kawaida.
Bomba hilo la inchi 8, lilisababisha kukosekana kwa huduma ya majisafi kwa takribani wakazi 900 wa Mihande, Vikuruti, Miswe na Mbwawa wa Mji wa Mlandizi, Tarafa ya Kibaha Vijijini.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa maboresho hayo, Mhandisi Ramadhani Mkata amesema mara kwa mara wakazi wa Mihande wamekuwa wakipata changamoto ya huduma ya maji kutokana na hitilafu inayojitokeza katika miundombinu ya maji.
Amesema baada ya matengenezo haya hakutakuwa na malalamiko ya wateja kwa kukosa huduma.
“Tumefanya maboresho ya miundombinu ya huduma katika bomba la inchi nane linalopeleka maji katika maeneo ya mbwawa ili kuimarisha huduma kwa wakazi wa maeneo hayo ambao walikuwa hawapati huduma ya maji mara kwa mara," amesema Mhandisi Ramadhani.
Amesema DAWASA ina mipango ya kuendelea kuboresha miundombinu ya maji katika maeneo mengine ya mkoa ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi kwa wote.
Naye Saida Omary, mkazi wa Miswe, ameiomba Mamlaka kuendelea na uboreshaji wa miundombinu hata katika mitaa mingine ili kuimarisha huduma hii muhimu kwa watu wote.
“Kitu kilichofanyika kwa sasa ni kizuri sana, niwaombe DAWASA kuendelea na zoezi hili katika mitaa mingine ili huduma ya maji izidi kuwa bora kwa kila siku,” amesema Ndugu Saida.
Mamlaka inaendelea na zoezi la uboreshaji wa miundombinu ya huduma ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji.
