DAWASA YAIMARISHA ULINZI NA USALAMA WA AFYA ZA WANANCHI KUPITIA WAUZA MAJI BINAFSI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Bodi ya Bonde la Maji la Wami/Ruvu, inaendelea na zoezi la utambuzi na ukaguzi wa visima na magari binafsi yanayouza maji Dar es Salaam na Pwani ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kulinda afya na usalama wa wananchi.
Zoezi hilo endelevu katika maeeneo yote ya Kihuduma, limetekelezwa katika maeneo yenye visima binafsi Boko Basihaya na Kituo cha Kuchota Maji kwa magari (Maboza) cha Mapinga limehusisha ukaguzi wa miundombinu ya maji, visima, magari ya maji, matanki pamoja na upimaji wa usalama wa maji na matibabu pale inapobidi.
Akizungumza katika zoezi hilo, Afisa Ubora wa Maji DAWASA, Ndugu Maliweza Shusha amesema zoezi hili linalenga kulinda na kuhakikisha usalama wa afya za watumiaji maji.
"Zoezi hili linatusaidia kujua ubora wa maji na kuhakiki usafi wa magari yanayobeba maji kwenda kwa wananchi, magari ambayo hayajakidhi viwango tunakubaliana yasafishwe na tunayafanyia matibabu kisha kuyawekea stika maalum ambazo zitamsaidia mteja kujua gari lililomletea maji limekaguliwa na linatoka katika chanzo salama," amesema Maliweza.
Naye Mtaalamu wa Maji chini ya Ardhi kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Ndugu Omary Hashim amesema ni wajibu wa Bonde kuhakikisha taratibu za uchimbaji na matumizi ya visima zinazingatiwa.
"Tunashiriki zoezi hili la ukaguzi wa visima ili kutoa elimu juu ya taratibu za kumiliki visima, utoaji vibali na kupima ubora wa maji ili kuhakikisha walaji wanapata na kutumia maji yenye ubora na viwango vinavyostahili kwa mujibu wa sheria ili kulinda afya na usalama wa wanufaika wa maji hayo ya visima," amesema Ndugu Hashim.
Kwa upande wake Mhandisi Mwandamizi wa Maji na Usafi wa Mazingira, EWURA, Kanda ya Mashariki l, Ndugu Ngugu David Linda ameelezea umuhimu wa zoezi hilo.
"EWURA tunafuatilia utekelezaji wa maagizo mbalimbali tuliyotoa ikiwa ni pamoja na DAWASA kuhakiki usajiri wa magari yanayotoa huduma ya maji, kupima Ubora wa Maji yanayosambazwa na magari ili kuendelea kulinda afya za walaji wakati huu wa ukame" Amesema Mhandisi Linda.
Zoezi hili maalum linalenga kuhakikisha wananchi wanapata maji salama na yenye ubora kutoka vyanzo vinavyotambulika ili kulinda afya zao hususan katika kipindi cha changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji iliyotokana na kupungua kwa uzalishaji katika Mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu.
