Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAIMARISHA USALAMA WA MAJI KUPITIA WATOA HUDUMA BINAFSI
23 Dec, 2025
DAWASA YAIMARISHA USALAMA WA MAJI KUPITIA WATOA HUDUMA BINAFSI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea kutekeleza zoezi la ukaguzi, upimaji na kutibu maji yanayotumika kwa wananchi kupitia visima binafsi vinavyotumiwa kwa dharura wakati huu wa upungufu wa maji uliopo maeneo mbalimbali ya kihuduma Dar es Salaam na Pwani.

Katika zoezi hilo, DAWASA kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) na Wasimamizi wa Bonde la Wami/Ruvu wametembelea maeneo mbalimbali yenye visima na magari binafsi yanayosaidia kuhudumia maji kwa wananchi ili kupima ubora wa maji na kutoa ushauri kiusalama kwa maji hayo yanayotumika katika kipindi hiki cha dharura.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo katika Kata ya Msigani, Afisa Mawasiliano wa DAWASA, Ndugu Jamal Chuma amesema Mamlaka inatekeleza zoezi hili muhimu ili kuhakikisha wananchi wanatambua na kutumia maji yaliyo salama kwa afya zao.

"Mamlaka inaendelea kusimamia na kufuatilia hali ya usalama wa maji yanayopatikana kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa, tunatembelea maeneo yenye visima na magari binafsi ili  kupima maji kimaabara, kutibu, kushauri pamoja na kuelimisha jamii juu ya kuzingatia matumizi ya maji safi na salama kwa kulinda afya zao hususan katika kipindi hiki cha uhaba wa maji," amesema Ndugu Chuma.

Kwa upande wake, Meneja wa Maabara Kuu ya Ubora wa Maji Dar es Salaam, Ndugu Hashim Kabelwa amewasihi wananchi kuwa makini na kuzingatia usalama wa maji wanayotumia ili kulinda afya zao.

"Kutokana na ukame uliopo, kuna watu wasio waaminifu wanaweza kusambaza maji yasiyo salama kiafya na kusababisha mlipuko wa magonjwa, hivyo tunawajibika kukagua miundombinu na kupima usalama wa maji kwa watoa huduma binafsi na kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanatambua chanzo cha maji wanayotumia kiwa kimehakikiwa na Mamlaka ili kuepuka madhara na milipuko inayoweza kujitokeza," amesema Ndugu Kabelwa.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Temboni, Kata ya Msigani, Ndugu Daniel Mwakyusa ameipongeza DAWASA na Wizara ya Maji kwa kufuatilia kwa karibu usalama wa maji kwa kupita katika mitaa yenye changamoto zaidi na kuchukua hatua na kushauri juu ya usalama wa maji.

Zoezi hilo linaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya kihuduma ikiwa ni kuendeleza jitihada za Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama wakati wa kipindi hiki cha uhaba wa maji uliotokana na kupungua kwa uzalishaji maji katika Mto Ruvu.