DAWASA YAINGIA MTAA KWA MTAA KUZITATUA CHANGAMOTO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mkoa wa Kihuduma Kibamba umefanya ziara ya mtaa kwa mtaa katika Kata ya Kiluvya, Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kutatua changamoto na kuboresha huduma ya majisafi.
Zoezi hilo limeongozwa na Meneja wa DAWASA Kibamba, Mhandisi Mkashida Kavishe akiambatana wa watumishi wengine wa Mamlaka.
"Lengo letu ni kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto yeyote inayojitokeza, lengo likiwa kuhakikisha tunaboresha huduma ya majisafi na kumaliza malalamiko yasiyo ya lazima," amesema Mhandisi Kavishe.
Amesema maeneo yote yanayopata maji kwa msukumo mdogo ikiwemo mtaa wa Justice, Umoja street na Kwa Shirima, Mamlaka inakwenda kufanya maboresho ya kuongeza msukumo wa maji na kumaliza changamoto hiyo.
Ndugu Ally Juma, mkazi wa mtaa wa Justice amesema wamefurahishwa na uamuzi wa uongozi wa DAWASA kufika mtaani kwao na kuangalia huduma ya maji lakini kuwasikiliza na kwapamoja kuona maneno ya kuboresha ili kila mmoja apate huduma bora ya majisafi.
"Maeneo yetu tulikuwa tunapata maji kwa msukumo mdogo, tunashukuru DAWASA kwakufika hapa ana kutusikiliza, sasa tunaimani kubwa tunaenda kupata huduma bora ya majisafi," amesema ndugu Ally.