Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAINGIA MTAANI BUZA, VITUKA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI
15 Oct, 2025
DAWASA YAINGIA MTAANI BUZA, VITUKA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI

Sehemu ya Watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imepita katika maeneo ya Buza na Vituka kuangalia hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Wameshuhudia uimarikaji wa huduma katika maeneo ya Makaburi ya City, Amani, Lumo, Kwa Gude na Ikizu pamoja na Mtongani kwa eneo la Vituka ambayo awali yalikuwa na changamoto ya huduma.

Akizungumza wakati wa zoezi la ufuatiliaji wa huduma ya maji katika maeneo hayo, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani DAWASA, CPA (T), Rosemary Lyamuya amesema kwa sasa huduma imerejea na maji yanapatikana muda mrefu na kwa presha kubwa.

"Siku chache zilizopita kulikuwa na changamoto ya maji lakini kwa sasa huduma imeimarishwa na maji yanapatikana na wananchi wanafurahia huduma," amesema Lyamuya.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Sigara, Ndugu Joseph Temba ameishukuru DAWASA kwa jitihada kubwa zinazoendelea kuimarisha huduma ya maji katika eneo lake.

"Hali ya maji imeanza kurudi vizuri. Tulikuwa na changamoto katika siku zilizopita lakini sasa maji yamefika na presha inaridhisha tunawashukuru DAWASA kwa kurejesha huduma hii muhimu," amesema Mwenyekiti Temba.

Kwa upande wa mkazi wa Makaburi ya City, Ndugu Tausi Abdulaziz ameishukuru Mamlaka kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha huduma ya maji wanaipata kwa uhakika kila mara.

Mamlaka inatoa wito kwa wananchi wanaopata changamoto za kihuduma kuwasiliana na DAWASA 181 (Bila Malipo) au 0735 202 121 (WhatsApp tu).