Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAINGIA MTAANI KUFUATILIA UIMARIKAJI WA HUDUMA
04 Jul, 2025
DAWASA YAINGIA MTAANI KUFUATILIA UIMARIKAJI WA HUDUMA

Hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi imeendelea kuimarika katika maneno mbalimbali ya Mkoa wa Dar Es Salaam na Pwani mara baada ya kukamilika kwa matengenezo kinga ya miundombinu ya umeme yaliyodumu kwa Saa 10 na kusababisha kuzimwa kwa Mtambo wa Ruvu Juu na Ruvu Chini. 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) imeingia mtaani kufuatilia upatikanaji na uimarikaji wa huduma, huku wakitoa wito kwa Mamlaka kuendelea kuboresha huduma kwa kutoa muda mrefu wa kuhifadhi maji pindi wanapoamua kufanya matengenezo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambangwa, Kata ya Mwananyamala Ndugu Mkakata Abdul ameeleza kuwa wananchi walipata adha za kukosa huduma kwa siku mbili (Julai 1 na 2, 2025 ) lakini kwasasa huduma imerejea na wananchi wa eneo lake wanapata huduma ya majisafi kwa kiwango kizuri.

Hafia Ibrahim, Mkazi wa mtaa wa Kambangwa - Mwananyamala amesema kuwa huduma ya maji imerejea lakini bado baadhi ya majirani hawajapata huduma na wengine wanapata kwa msukumo mdogo. 

"Tulipokea taarifa ya kukosekana kwa huduma ya maji kutoka DAWASA kwa wiki hii mapema, lakini kuanzia jana asubuhi (Julai 2,2025) huduma imerejea kwa msukumo mzuri. Wananchi tunaendelea na shughuli zetu za kila siku za kijamii na kiuchumi,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Bi Everlasting Lyaro amekiri kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji kwa zaidi ya saa 10 kwa siku za (Jumatatu hadi Jumanne), lakini kwa sasa huduma imerejea na kuwapa uhakika wananchi wote kuwa watapata maji, huku akiwasisitiza mafundi wa Mamlaka kukesha mtaani kufuatilia huduma.

"Mamlaka ilitangaza matengenezo yaliyodumu kwa saa 10 na kufika siku ya Julai 2, tuliwasha mitambo yetu ya uzalishaji maji ya Ruvu Juu na Chini na huduma kuanza kurejea kwa wananchi. Leo tunapita mitaani kuhakikisha huduma imeimarika kwa kiasi gani na kuangalia maeneo ambayo bado yana changamoto ili tuweze kuzitatua ” ameeleza Bi Lyaro.