Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAJA NA MIKAKATI UPUNGUFU WA MAJI
14 Dec, 2025
DAWASA YAJA NA MIKAKATI UPUNGUFU WA MAJI

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb)amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA inaendelea na mkakati wa kuhakikisha huduma ya majisafi inaimarika na kupatikana kwa wananchi wote ili kukabiliana na upungufu wa maji. 

Amesema kuwa changamoto iliyopo ya maji ni kutokana na kuchelewa kwa mvua za masika zilizotarajiwa kunyesha kwa kipindi cha mwezi wa kumi na mwezi wa kumi na moja. 

Mhe. Aweso amekumbushia maagizo mahususi aliyoyatoa kwa Mamlaka ya kuhakikisha kiasi cha maji kilichopo kwa sasa kinagawanywa kwa wananchi kwa usawa kulingana na ratiba ya usambazaji maji inavyoelekeza. 

"Wananchi wapate maji ipasavyo kulingana na ratiba ya usambazaji inavyoelekeza ili kila mwananchi apate maji japo kwa saa chache," ameeleza. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire ameeleza sababu zilizosababisha changamoto hii kuwa ni pamoja na kuchelewa kwa mvua za vuli zilizotarajiwa kunyesha katika mwezi wa kumi hadi mwezi wa kumi na mbili. 

Pia ni kutokana na Mto Ruvu kuacha njia yake ya mwelekeo wa maji katika maeneo ya Kitomondo na kutengeneza mchepuko unaotawanyisha maji na kupunguza kiasi cha maji Mtoni. 

Ameongeza kwa kusema kuwa ongezeko la shughuli za kilimo ni mojawapo ya sababu zilizosababisha kuharibika kwa chanzo cha maji kwa kuathiri mwelekeo wa maji ya Mto Ruvu. Hivyo jitihada kubwa zinahitajika katika kukabiliana na changamoto hii. 

Mbali na hapo Mhandisi Bwire amesema Mamlaka imechukua hatua mbalimbali za kuboresha hali hii ikiwemo kufufua visima vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya Jiji ili viweze kutumika kama mbadala wa kuongeza upatikanaji wa majisafi kwa wananchi. 

"Tunajitahidi kuongeza nguvu kubwa katika kudhibiti upotevu wa maji mitaani ili maji yanayopotea yaweze kuingia kwenye mfumo na kuhudumia wananchi," amesema Mhandisi Bwire. 

Naye Mkurugenzi wa Bonde la Maji Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi amebainisha kuwa upungufu wa maji katika Mto Ruvu umesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi linalosababisha ongezeko la joto la wastani wa digrii 2.3. 

Amesema hatua zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na kusitisha utoaji wa vibali kwa Watumiaji wa skimu za umwagiliaji hususani katika kipindi hiki cha kiangazi.