Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAKARIBIA KUMALIZA ADHA YA MAJI NZASA, SOMELO NA ZINGIZIWA
22 Jul, 2026
DAWASA YAKARIBIA KUMALIZA ADHA YA MAJI NZASA, SOMELO NA ZINGIZIWA

Takribani wakazi 17,200 wa maeneo ya Nzasa, Somelo na Zingiziwa katika Wilaya ya Ilala wanatarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama baada ya Mradi wa Maji wa Nzasa–Somelo kufikia asilimia 95 ya utekelezaji.

Mradi huo unahusisha uchimbaji wa kisima kipya cha maji katika eneo la Ofisi ya Kata ya Zingiziwa, ambacho kinatarajiwa kuzalisha takribani lita 115,000 za maji kwa saa, hatua itakayoongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo hayo.

Mradi wa Nzasa–Somelo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkandarasi B2G, chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri WAPCOS.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Stephen Urio, amesema mradi unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia (World Bank) kwa gharama ya Shilingi bilioni 2.3.

Amesema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita milioni mbili, ulazaji wa mabomba ya inchi 12 yenye urefu wa kilomita 4.4, ujenzi wa jengo la pampu pamoja na chemba za valvu, ambazo zinaendelea kukamilishwa.

> "Lengo letu ni kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika. Kazi zinaendelea vizuri na tunasimamia kwa karibu viwango vyote vya ubora vilivyowekwa," amesema Mhandisi Urio.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Zingiziwa, Erick Ishengoma, amesema kwa muda mrefu wakazi wa kata hiyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, lakini utekelezaji wa mradi huo umeleta matumaini mapya.

"Tunashukuru juhudi za Serikali za kuhakikisha hata wananchi wa maeneo ya pembezoni wanapata huduma ya maji safi na salama. Tunaipongeza DAWASA kwa ushirikishwaji wake na hatua inazochukua kutatua changamoto ya maji katika eneo letu," amesema Ishengoma.

Naye mkazi wa Mtaa wa Ngobedi, Zingiziwa, Leila Kipuga, amesema kukaribia kukamilika kwa mradi huo kunawapa matumaini ya kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hasa nyakati za asubuhi.

"Tulipopata taarifa za mradi huu tulijawa na furaha kwa sababu tulijua changamoto ya maji itaenda kuwa historia. Tunaomba DAWASA ikamilishe kazi hii haraka ili nasi tuanze kunufaika na huduma ya maji safi katika makazi yetu," amesema.

Mradi huo unatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu la upatikanaji wa maji kwa maelfu ya wakazi wa Nzasa, Somelo na Zingiziwa, huku ukiimarisha huduma ya maji katika maeneo yanayokua kwa kasi ndani ya Wilaya ya Ilala.