Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAONGEZA WIGO WA WADAU MUHIMU KIGAMBONI
11 Nov, 2024
DAWASA YAONGEZA WIGO WA WADAU MUHIMU KIGAMBONI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefungua klabu ya utunzaji wa mazingira katika Shule ya Msingi ya Gomvu, iliyopo Kigamboni kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uwezo wa namna bora ya kutumia maji na kutunza mazingira. 

Bi Hashura Kamugisha, Afisa Mawasiliano amesema kuwa dhumuni la kuanzisha klabu za mazingira katika ngazi za shule za Msingi na Sekondari, ni kutengeneza kizazi bora kinachofahamu umuhimu wa maji, utunzaji wa mazingira na namna bora ya kutunza vyanzo na miundombinu ya maji ili kuweza kuwa na huduma ya maji endelevu. 

“Leo tumefungua klabu ya mazingira mpya katika shule hii kwa lengo la kuendeleza jitihada za Mamlaka katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu maji kwa ujumla, hasa kwa wanafunzi ili kuwa na kizazi bora kinachojua umuhimu wa maji katika jamii. Hivyo, ni jukumu lao pia kutambua vyanzo vya maji na miundombinu na namna ya kuvitunza kwa ustawi wa jamii nzima," ameeleza Bi Hashura. 

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Mwalimu Noel Myunga James ambae ni mlezi wa klabu ya Mazingira shuleni hapo, ameishukuru DAWASA kwa jitihada za kufikia jamii hasa kwa watoto wa shule za msingi na kutoa elimu ya maji na usafi wa Mazingira akiamini itakuwa chachu ya kueneza elimu hii kwa jamii. 

“Elimu ya maji na usafi wa Mazingira ni muhimu katika jamii, kwa kuanzisha klabu hizi mashuleni italeta mabadiliko ya kitabia katika masuala mazingira na matumizi sahihi ya maji hivyo tunaishukuru sana DAWASA kwa jitihada za kutoa elimu hiyo kwa vijana wetu hakika ni adhina ya kudumu,” amesema Mwl. Myunga. 

Nae Fathiya Kassim, mwanafunzi na mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa mazingira ya shuleni hapo, ameishukuru Mamlaka kwa kuwa mlezi na kutoa nafasi ya wao kujifunza mambo mbalimbali ya Maji na Usafi wa Mazingira.