DAWASA YASHIRIKI UTIAJI SAINI MIKATABA YA UTENDAJI SEKTA YA MAJI NCHINI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeungana na Bodi za Maji za Mabonde sambamba na Mamlaka za Maji Nchini kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya utendaji kazi ya uwajibikaji kwa kuzingatia matokeo utakaolenga kuboresha huduma za Maji Nchini.
Hafla hiyo iliongozwa na Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb.) amesisitiza umuhimu wa watendaji wa Sekta ya Maji kuacha alama kwa kuzingatia matokeo, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Waziri Aweso amesema mikataba ya utendaji ni nyenzo muhimu ya kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha taasisi za sekta ya maji zinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Waziri Aweso amezitaka taasisi za sekta ya maji kuongeza kasi ya utekelezaji katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa kuimarisha utawala bora, kuongeza uzalishaji wa maji, kudhibiti upotevu wa maji, kupunguza malalamiko ya wateja na kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Tukio hilo limeshuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka Mhandisi Mkama Bwire.
