Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YATAMBULISHA MRADI WA MAJI BUYUNI - KIGAMBONI
10 Jan, 2025
DAWASA YATAMBULISHA MRADI WA MAJI BUYUNI - KIGAMBONI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA), imetambulisha  mradi wa maji maeneo ya pembezoni  kwa Wananchi wa Mtaa wa Buyuni katika Kata ya Pembamnazi Wilaya ya Kigamboni ulioanza kutekelezwa Oktoba, 2024

Utambulisho huo umefanyika katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Soko la Samaki katika Mtaa wa Buyuni Kata ya Pembamnazi uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Tawala Wilaya ya Kigamboni.

Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Baraka Masolo amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maji imekusudia kutekeleza miradi ya  kusambaza maji kwa maeneo ya pembezoni kwa lengo la kufikisha huduma ya maji kwa kila  Mwananchi na Wilaya ya Kigamboni ikiwa ni mojawapo.

Utekelezaji wa mradi huu ambao ni maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe Kassim Majaliwa alipotembelea Wilaya ya Kigamboni mapema tarehe 6.10.2025 na kuagiza kupeleka huduma ya Majisafi katika kata nne za Pembamnazi,Kimbiji, Kisarawe II na Somangila.

“Mradi huu wenye Gharama ya Shilingi Milioni 254 hadi sasa umefikia asilimia 60 ya utekelezaji wake na baadhi ya maeneo wamekwisha anza kupata huduma na unatarajia  kukamilika Februari 2025 na kuhudumia wakazi 23,724". Alisema Masolo.

Aidha, katika kutekeleza mradi huo katika kata nne za mwanzo kazi  zinazotekelezwa ni uchimbaji  na ulazaji wa Mabomba kwa umbali wa Kilomita 11, ujenzi wa matanki ya maji yenye lita za ujazo 20,000, ujenzi wa  vituo 14 vya kuchotea maji, kukarabati mnara wa maji wenye uwezo wa kubeba Lita 10,000 na kufunga pampu ya kusukuma maji.

Mradi wa maji katika maeneo ya pembezoni  inafanyika katika kata za Pembamnazi, Somangila, Kisarawe II na Kimbiji katika mitaa ya Mwasonga, Mwaninga,Mbutu Kichangani ,Kwa Chale na Buyuni.